Jumuiya ya Kimataifa tarehe 20 Juni inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani. Takwimu
zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 45 wanaolazimika kuzikimbia nchi zao
ili kutafuta maisha bora zaidi ugenini. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Barani
Ulaya, Caritas Europe linasema kwamba, kuna maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali
za dunia wanaoingia Barani Ulaya kwa njia ya Bahari.
Hawa ni watu wanaotafuta
kimsingi: amani, utulivu, demokrasia, utu na maendeleo yao. Hii ni changamoto kwa
Nchi za Ulaya kuhakikisha kwamba, zinatengeneza sera na mikakati inayojikita katika
ukarimu, udhibiti na ushirikishwaji katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji
wanaowasili kila siku Barani Ulaya. Nchi za Ulaya ziweke sheria ambazo zitawawezesha
watu kuhamia kihalali, kuliko mtindo wa sasa wa kuwa na kundi kubwa la wahamiaji haramu.
Wahamiaji
wanaotafuta fursa za ajira wapewe vibali; wale wanaokimbia vita na majanga asilia
wapokelewe kwa heshima na kwamba, vibali viwasaidie wahamiaji hawa kuwa na uhuru wa
kutembea. Kuna kundi kubwa la wahamiaji linalihifadhiwa nchini Italia.
Caritas
inatambua ukarimu, lakini pia inakiri shida na magumu wanayokabiliana nayo wahamiaji
hawa huko kambini. Ili kukabiliana na changamoto hii kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
kusaidiana kwa hali na mali, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe
wake kwa Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2014.