Ukosefu wa uhuru wa kidini unahatarisha amani, maendeleo na mshikamano wa watu!
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaonesha utajiri mkubwa unaofumbatwa katika
Historia ya Kanisa kwa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini, kwa kutambua
kwamba, kil mtu ni muasisi wa ukweli kuhusu asili na hatima ya maisha yake. Ndani
mwake kuna maswali na mawazo ambayo kamwe hayawezi kuchakachuliwa kwa vile yanapata
chimbuko lake kutoka katika undani wa utu wake mwenyewe.
Haya ni masuala ya
kidini na uhuru wa kuabudu yanayojitokeza daima katika maisha ya mwanadamu, kwa kuonesha
umuhimu wake, uhusiano na ulimwengu, historia na kuondoa giza linaloyasakama maisha
ya binadamu, kwani mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Hii ni sehemu
ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 20 Juni 2014 wakati
alipokuwa anazungumza na wajumbe wa kongamano la kimataifa lililokuwa linafanyika
kwenye Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma kuhusu "uhuru wa kidini mintarafu
sheria za kimataifa pamoja na kinzani za tunu msingi za maisha".
Uhuru wa kidini
ni haki msingi inayoonesha utu unaomsukuma mwanadamu kutafuta ukweli na kuukumbatia
kwa kutambua nguvu iliyomo ndani mwake inayoweza kumsaidia kutumia uwezo wake wote.
Uhuru wa kidini ni mchakato unaomwezesha mtu kuishi mintarafu kanuni msingi za kimaadili
zinazobubujika kutokana na ukweli uliopatikana katika maisha binafsi au katika hadhara.
Uhuru wa kidini ni kati ya changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi
ambamo mawazo dhaifu yanaonekana kutawala zaidi kwa kisingizio cha maridhiano, hali
ambayo wakati mwingine inapelekea madhulumu kwa wale wanaosimama kidete kulinda na
kumtetea mwanadamu na kanuni maadili.
Sheria za kimataifa na kitaifa zinapaswa
kutambua na kutetea uhuru wa kidini ambao kimsingi ni sehemu ya utu wa binadamu inayomwezesha
kuwa kweli huru na kwamba, hiki ni kiashiria cha demokrasia na kanuni msingi ya uwepo
wa Serikali yoyote ile! Uhuru wa kidini ukitambuliwa na kusimamiwa kikamilifu ni chachu
ya maendeleo na mahusiano bora katika jamii, serikali na dini mbali mbali. Hapa dini
na serikali zinaweza kushirikiana kwa dhati bila ya kuingiliana katika majukumu yake.
Mmong'onyoko
wa tunu msingi za kimaadili unaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia kanuni msingi zinazokubalika
na wengi, ili kudumisha mshikamano kwa ajili ya mafao ya wengi. Lakini ukweli wa mambo
unaonesha kwamba, leo hii bado kuna udhibiti mkubwa wa haki msingi za binadamu na
ubaguzi unaotokana na mwelekeo wa imani ya mtu, kiasi kwamba, hata wakati mwingine,
kumekuwepo na madhulumu na nyanyaso za wazi kabisa, mambo yanayochafua akili, amani
na hatimaye kunyanyasa utu wa binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba,
kwa bahati mbaya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ndilo kundi ambalo limeendelea
kunyanyaswa, kudhulumiwa na kutengwa, hali ambayo kwa nyakati hizi inaonekana kuongezeka
maradufu kuliko hata ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo, tangu wakati ule Costantino
alipochapisha Waraka wa uhuru wa kidini kwa Wakristo.
Ni matumaini ya Baba
Mtakatifu Francisko kwamba, kongamano hili litasaidia kupambanua hoja za kisayansi
na sababu zinazotaka sheria kuheshimu na kulinda uhuru wa kidini.