Baraza la Maaskofu Katoliki Canada hivi karibuni limemwandikia barua Waziri mkuu wa
Canada Bwana Stephen Harper kumtaka kusimamia kwa dhati kabisa sera na mikakati ya
kisiasa inayojikita katika kutafuta mafao ya wengi na kutetea zawadi ya uhai tangu
pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika
kadiri ya mapendi ya Mungu.
Wanasiasa
wanapaswa kuwa mwelekeo mpana katika utekelezaji wa majukumu yao si tu nchini Canada
bali pia kwa kuangalia ustawi na maendeleo ya dunia inayowazunguka.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Canada linasikitika kusema kwamba majadiliano ya kisiasa yanayoendelea
nchini humo kuhusu utakatifu wa maisha, hususan mtoto anapotingwa mimba tumboni mwa
mama yake na mwisho wa maisha ya mwanadamu ni mambo ambayo hayaendi sawasawa, kwani
wanasiasa wanataka kuweka rehani zawadi ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo.
Hali hii inadhalilisha utu na heshima ya binadamu, jambo ambalo haliwezi kukubalika
kamwe!
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kwa mtazamo mpana linajaribu kupembua
hali ya kiuchumi sehemu mbali mbali za dunia kwa kusema kwamba, athari za myumbo wa
uchumi kimataifa zinaendelea kuwatendea watu wengi duniani kwa kukosa fursa za ajira
na hivyo kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa familia na jamii husika.
Athari
za mabadiliko ya tabianchi ni mzigo mkubwa kwa nchi zinazoendelea duniani kiasi kwamba
watu wengi wanaendelea kutumbukizwa katika lindi la umaskini au kulazimika kuzikimbia
nchi zao na matokeo yake, watu wengi wanaendelea kupoteza maisha kwa kufa maji baharini
au jangwani kabla ya kufikia ndoto zao za maisha bora zaidi. Vita na ukosefu wa amani
na usalama ni mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuyashughulikia kwa kina
na mapana, vinginevyo dunia hii itaendelea kuwa ni uwanja wa fujo, ikitawaliwa na
falsafa ya “mwenye nguvu mpishe”.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakumbuka
mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka ishirini iliyopita; vita inayoendelea
kupukutisha maisha ya watu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Sudan ya Kusini
bila kusahau vitendo vya kigaidi ambavyo vinaendelea kuitikisa Nigeria na sehemu nyingine
za Bara la Afrika. Kuna kundi kubwa la watu ambalo limetekwa nyara huko Nigeria na
Cameroon. Yote haya ni matukio yanayohitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili
kuweza kupata suluhu ya kudumu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaishukuru
Serikali kwa msaada wake wa hali na mali kwa ajili ya wananchi wa Syria wanaoteseka
kutokana na vita pamoja na mikakati ya Serikali katika kulinda na kudumisha uhuru
wa kuabudu huko Mashariki ya Kati. Wanaiomba Serikali kuendelea kufanya maboresho
katika sheria za uhamiaji pamoja na kusaidia mchakato wa upatikanaji wa amani nchini
Venezuela.
Katika masuala ya kimataifa, Maaskofu wanaendelea kukazia umuhimu
wa kujikita katika mchakato wa kidiplomasia na majadiliano yanayojikita katika ukweli
na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi. Vita na matumizi ya nguvu ni sera ambazo zimepitwa
na wakati n ani chanzo kikuu cha maafa na kikwazo cha maendeleo ya binadamu. Jumuiya
ya Kimataifa haina budi kujikita katika kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu, ili
kukoleza haki na amani mambo muhimu sana katika ujenzi wa jamii yoyote ile!
Imeandaliwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.