2014-06-19 09:02:21

Ratiba elekezi ya Papa Francisko nchini Korea: 14 - 18 Agosti 2014!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuanza hija yake ya kichungaji nchini Korea ya Kusini kuanzia tarehe 14 hadi 18 Agosti 2014 ili kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Vijana wa Bara la Asia litakalofanyika Jimboni Daejeon kwa kuongozwa na kauli mbiu "Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia".

Hii itakuwa ni hija ya tatu kimataifa kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, mwaka mmoja uliopita. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani, kwani itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu alitangaza nia hii wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Siku ya Vijana Kijimbo Mwaka 2014, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican baada ya kukabidhi Msalaba wa Vijana kwa Vijana kutoka Jimbo kuu la Krakovia, Poland, watakaokuwa wenyeji wa Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016.

Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma, Jumatano tarehe 13 Agosti 2014 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Fumicino na kuwasili nchini Korea ya Kusini tarehe 14 Agosti 2014 majira ya asubuhi. Ratiba inaonesha kwamba, hakutakuwa na mapokezi rasmi kwenye Uwanja wa Ndege, badala yake, Baba Mtakatifu atakwenda moja kwa moja hadi kwenye Ubalozi wa Vatican na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kupata mapumziko mafupi. Alasiri atamtembelea Rais wa Korea ya Kusini, Ikulu na hapo kutafanyika mapokezi rasmi ya Kiserikali na baadaye, Baba Mtakatifu atazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea na hivyo kufunga ukurasa wa siku ya kwanza ya hija yake ya kitume nchini Korea ya Kusini.

Ijumaa, tarehe 15 Agosti 2014, Baba Mtakatifu atakwenda Jimboni Daejeon kwa Helkopta hadi kwenye Uwanja wa Michezo Kimtaifa na hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho. Wakati wa chakula cha mchana, Baba Mtakatifu anatarajiwa kushiriki pamoja na wawakilishi wa vijana kutoka Asia watakaokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya Kongamano la sita ya Vijana Barani Asia. Jioni atazungumza na Vijana kutoka Asia watakaokuwa wamekusanyika kwenye Madhabahu ya Solmoe na baadaye, Baba Mtakatifu atarejea tena mjini Seoul kwa mapumziko.

Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2014, Baba Mtakatifu Francisko atakwenda kusali kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Korea yaliyoko Seo So mun na hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza mtumishi wa Mungu Paul Ji-Chung na wenzake 123 kuwa Wenyeheri. Hawa ni mashahidi waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kunako karne ya kumi na nane. Ibada hii itafanyika kwenye Lango kuu la Seoul, lijulikanalo kama Gwanghwamum.

Majira ya jioni, Baba Mtakatifu atatembelea kituo cha walemavu Jimbo kuu la Seoul, kilichoko Kkottognate na kuzungumza na Watawa pamoja na viongozi wa utume wa walei nchini Korea, kabla ya kurejea tena mjini Seoul.

Jumapili asubuhi tarehe 17 agosti 2014, Baba Mtakatifu atakutana na Maaskofu Katoliki kutoka Barani Asia kwenye Madhabahu yaliyoko mjini Haemi na baadaye atapata nao chakula cha mchana na jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga rasmi Kongamano la Sita la Vijana Barani Asia kwa Mwaka 2014.

Jumatatu asubuhi, kabla ya kuanza safari yake ya kurudi mjini Vatican, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa kidini katika Kanisa kuu la Jimbo kuu la Seoul. Hapa ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho na hili ndilo tukio litakalohitimisha hija yake ya kichungaji nchini Korea ya Kusini.









All the contents on this site are copyrighted ©.