2014-06-19 08:14:32

Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja, kifungo cha upendo!


Siku kuu ya Ekaristi Takatifu husherehekewa kwa Ibada na maandamano makubwa mitaaani ili kumtolea ushuhuda Yesu Kristo aliyeamua kuendelea kubaki kati ya wafuasi wake katika maumbo ya Mkate na Divai. RealAudioMP3

Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu ya Yesu Kristoaliyoianzisha ili kudumisha sadaka ya Msalaba kwa karne zote mpaka atakaporudi katika utukufu. Kwa namna hii alilikabidhi Kanisa ukumbusho wa kifo na ufufuko wake.

Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja, kifungo cha upendo, Karamu ya Pasaka ambamo Kristo anajisadaka kama chakula cha uzima wa milele, ili kuijaza roho neema na hapo mwamini anapewa amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya kikristo. Katika Ekaristi kazi ya Mungu ya kutakasa na ibada ya waamini zinafikia kilele chake, kwani humu kuna mema yote ya maisha ya kiroho yaani Kristo mwenyewe anayejitoa sadaka ya Pasaka.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe katika wake maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kwa Mwaka 2014 linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga fursa za matumaini. Siku kuu hii kwa mwaka 2014 inaadhimishwa hapo tarehe 22 Juni na kwa upande wa Hispania ni siku pia ya kuonesha mshikamano wa upendo, kwani Ekaristi takatifu ni Fumbo la Upendo na Matumaini, changamoto na mwaliko wa kufungua macho ili kuona mahitaji ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wawe makini kusikiliza kilio cha wenye njaa na kiu ya haki, ili waweze kuwajengea matumaini mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Maaskofu wanawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia hali halisi ya maisha ya watu badala ya kupima mafanikio ya kiuchumi kwa kipimo kinachotolewa na Makampuni makubwa, mikopo kutoka Benki, faida inayopatikana katika soko la bidhaa na huduma pamoja na uwekezaji katika miradi mbali mbali. Haya ni mambo msingi, lakini kwa bahati mbaya ni sera na mikakati inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa fedha badala ya utu na heshima ya binadamu.

Hapa kuna kundi kubwa la wafanyakazi wasiokuwa na fursa za ajira, watu ambao utu wao umewekwa rehani kutokana mtikisiko wa uchumi kimataifa; watu wengi wanaendelea kutumbukizwa katika baa la umaskini wa hali na kipato kutokana na Serikali kuendelea kubana matumizi katika maboresho ya huduma za kijamii. Maaskofu Katoliki Hispania wanasema, hapa kuna haja ya kuwaangalia maskini kwa jicho la kimungu.

Miaka sita tangu myumbo wa uchumi kimataifa utokee hali ya maisha ya watu wengi imeathirika vibaya, kuna baadhi ya watu wanatengwa ndani ya jamii hali ambayo inaendelea kusababisha makundi ya watu ndani ya jamii; kuna baadhi ya watu wanafaidika na wengine “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanazidi kuongezeka zaidi na zaidi, hali ambayo ni mbaya zaidi miongoni mwa watoto nchini Hispania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linasema takwimu za Shirika la Kilimo na Chakula zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 845 wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani, jambo ambalo bado ni kashfa kwani ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi kuna chakula kingi kinachozalishwa duniani na baadhi ya watu wanakula na kusaza, lakini jambo la kushangaza ni kuwaona kwamba, hawaguswi hata kidogo na mahangaiko ya jirani zao, sehemu nyingine za dunia.

Watu waguswe na mahitaji ya wengine na kamwe wasioneshe shingo ngumu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajitahidi kuwajengea jirani zao nafasi za matumaini ili kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kwa njia ya mshikamano. Wananchi wajifunze kuwa na matumizi bora na sahihi ya chakula kwani chakula ni haki kwa wote. Upendo na mshikamano viwaongoze waamini kuwa kweli ni watu wa Ekaristi, watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao.

Watunga sera na wawekezaji wasaidie kuchangia katika mchakato wa uchumi unaojali, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uchumi usiomjali binadamu ni chanzo cha mahangaiko na kifo chake.

Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, washirikishwe katika maboresho ya uchumi kitaifa na kimataifa. Kila mtu atekeleze wajibu wake kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la umaskini duniani. Umefika wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga fursa za matumaini katika maisha kwa kukazia Injili ya Uhai, Haki na Udugu.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.