2014-06-19 11:23:16

Changamoto ya kusimama kidete kutangaza Injili ya Uhai na Utamaduni wa amani!


Makatibu wakuu kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE wameanza mkutano wao wa arobaini na mbili unaofanyika mjini Strasburg, Ufaransa kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 22 Juni 2014, kwa pamoja wakidhamiria kusimama kidete kuendeleza Injili ya Uhai na Utamaduni wa Amani. Baraza la Jumuiya ya Ulaya lina mchango mkubwa katika maamuzi mazito kwa wananchi wa Ulaya katika masuala ya kijamii na kitamaduni.

Mkutano huu unalenga kuwasaidia Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu kufahamu kwa kina na mapana mchango unaotolewa na Baraza la Ulaya katika masuala ya kidemokrasia, haki msingi za binadamu, amani na maendeleo endelevu ya binadamu: Uhai wa binadamu na uhuru wa kuabudu ni kati ya mambo ambayo ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe ni masuala ambayo yanapaswa kuangaliwa na kupewa uzito unaostahili kutoka kwa Baraza la Jumuiya ya Ulaya na Makanisa Barani Ulaya.

Itakumbukwa kwamba, Baraza la Umoja wa Ulaya linaundwa na nchi wanachama 47 zinazowakilishwa pia kwenye Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya. Ni Jumuiya ambayo inahistoria tofauti na kwa baadhi ya nchi historia yake imechafuliwa kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia, lakini Jumuiya ya Ulaya ina mizizi na chimbuko lake katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, historia ambayo ina zaidi ya miaka elfu mbili! Mkutano huu unafanyika kwa faragha!







All the contents on this site are copyrighted ©.