Caritas Mbeya inawashukuru wafadhili katika mapambano dhidi ya Ukimwi!
Hivi karibuni mkurugenzi wa Global Health program kutoka nchini Marekani, Bwana Tiffany
Hamm kwa kushirikiana na shirika la water Reed/HJFMRI imeipongeza Idara ya Caritas
na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya kwa juhudi zake za ari na mali za kupambana na
maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi katika jamii kwa shirikiana na serikali
ya Tanzania.
Mkurugenzi huyo aliongozana na ujumbe wa wafanyakazi wenzake watano
kutoka nchini Marekani ambao ni Sundha Srinagesh Mkurugenzi katika ofisi inayoshughulikia
masuala ya ufadhili, Meneja kutoka timu inayoshughulikia mikataba HJMRI Troy Hagrove
na Meneja program Eric Black.
Wengine ni pamoja na wafanyakazi wa Water Reed/HJFMRI
kutoka makao makuu ya Tanzania yaliyopo mkoani Mbeya wakiongozwa na Mkurugenzi wa
tanzania Klaus Sturbeck ambapo pamoja na mambo mengine wametembelea kuona shughuli
mbalimbali zinazofanywa na Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya kuhusu
masuala ya vita dhiti ya maambukizi ya ukimwi na ukimwi, Ukatili wa kijinsia, ukatili
kwa watoto pamoja na Saratani ya uzazi.
Tiffany amesema mashirika mengine
yanapaswa kuiga mfano wa Idara ya Caritas Mbeya kwa kufanyakazi wa kujitoa kwa moyo
wao wote na kwa nguvu zao zote kwa kushirikiana na jamii pamoja na serikali jambo
ambalo linaleta matumaini makubwa kwa watu wenye shida mbalimbali za kiafya hususani
maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi na saratani ya shingo ya kizazi.
Licha
ya kuwepo kwa jitihada za dhati za serikali kushirikiana na wafadhili kutoka nchi
mbalimbali kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na Ukimwi, bado kumekuwepo
na changamoto ambazo zinachelewesha harakati hizo ikiwemo umaskini,imani za kidini,
mila na desturi sanjari na watendaji wasio waaminifu na wasiozingatia maadili ya
kazi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Nkuyu, Kata ya Iganzo jijini Mbeya, Peter Mwamwaja
akijibu swali lililoulizwa na Mkurugenzi wa Shirika la Water Reed-Tanzania, Klaus
Sturbeck ametaja mojawapo ya changamoto wanayokumbana nayo kuwa ni baadhi ya watu
wanaojikuta wakiwa na maambukizi baada ya kupima kujisikia vibaya na hatimaye kukimbia
kwa kuhama mtaa mmoja na kukimbilia mwingine.
"Watu wanaona aibu wakishapima
na kupata majibu na wakijikuta wameambukizwa wanaondoka Iganzo na kuhamia pengine
Kata ya mwakibete,huko wanajificha na kuendeleza ngono na matokeo yake maambukizi
yanazidi kuongezeka, tunajitahidi kuwashauri na kuwashirikisha wahudumu wa Caritas
na tunafanikiwa,"anasema Mwenyekiti huyo.
Msimamizi wa huduma majumbani, Idara
ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya Upendo Mwaipopo naye anasema umaskini
kwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi na kujikuta wakipisha
siku bila kula ni mojawapo ya sababu inayowafanya baadhi yao kuacha kutumia dawa wakidai
zinawatesa tumboni na kuwamaliza nguvu. Ofisa afya ya jamii Kata ya Iganzo, Asteria
Kayange anaelezea namna anavyopambana na changamoto ya waathirika kujinyanyapaa baada
ya kubaini wanaishi na maambukizi kwa kujenga mazoea ya kuwa nao jirani na kuwashauri
kujikubali.
Mtendaji wa mtaa wa Nkuyu na Mwambenja, Mage Makwenda akifafanua
swali lililoulizwa na ujumbe huo endapo anaifahamu idara ya Caritas na maendeleo Jimbo
katoliki la Mbeya na baadhi ya wahudumu wake anasema wamekuwa wakifanyakazi kwa pamoja
na mawasiliano muda wote na amepongeza kwa wepesi wao wa kufika pindi wanapohitajika
kwa haraka.
Suala la mfumo dume katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi
vya ukimwi bado imekuwa ni changamoto kubwa kama ambavyo Mweka hazina wa kikundi cha
watu wanoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi cha Wemavinga, Kata ya Iganzo, Pendo
Machonga anavyosema kuwa suala la kupima afya ni na kila mmoja wetu na kuwataka wanaume
kuacha tabia ya kuwatumia wanawake kama kioo cha kujitazamia majibu ya afya zao.
Mratibu
wa kitengo cha Ukimwi, jinsia, wanawake na watoto ,Idara ya Caritas Jimbo Katoliki
la Mbeya Praxeda Manyuka amelishukuru Shirika la Water reed/HJFMRI na wafadhili wengine
kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuunga mkono harakati za kupambana
na maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Saratani ya kizazi, ukatili wa kijinsia
kwa wanawake na watoto.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Caritas na maendeleo
Jimbo Katoliki la Mbeya, Anthony Kisengo kwa niaba ya Mkurugenzi Edgar Mangasila amesema
kwa niaba ya Askofu Evaristus Marcus Chengula (IMC) anapenda kuwapongeza na kuwaomba
waendelea kusaidiana katika kuikomboa jamii. Mmoja wa viongozi wa kikundi cha uhamasishaji
cha vijana klabu kinachohudumiwa na Caritas Mbeya, Brown Isaya ametoa wito kwa serikali
na wadau wengine kuwasaidia kwa ari na mali ili waweze kufanikisha lengo la kutoa
hamasa kwa jamii kuhusu mapambano ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi.