Baba Mtakatifu mara baada ya Katekesi yake kuhusu Kanisa, amewakumbusha waamini na
watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 20 Juni 2014, Jumuiya ya Kimataifa itaadhimisha
Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2014. Hawa ni watu ambao wanalazimika kuzikimbia
nchi zao kutokana na kinzani pamoja na madhulumu.
Idadi ya wakimbizi duniani
inaendelea kuongezeka maradufu katika siku za hivi karibuni na kuna idadi kubwa ya
watu wanaotamani kuzikimbia nchi zao ili kusalimisha maisha yao! Kuna mamillioni ya
wakimbizi kutoka nchi na dini mbali mbali duniani wanaoishi katika majanga na madonda
makubwa ya kijamii ambayo pengine itakuwa vigumu sana kuweza kuponywa.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo
wa upendo na ukarimu kwa wakimbizi, kwa kushirikishana nao hofu na wasi wasi wa maisha
yao kwa siku za usoni na pale inapowezekana kuwasaidia katika mahangaiko yao.
Baba
Mtakatifu anawaombea watu na taasisi ambazo zinaendelea kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya kuonesha ukarimu na usalama, kwa kuwapokea na kuwatunza wakimbizi, huku
wakizingatia utu na heshima yao, kama sehemu ya mchakato unaolenga kuwapatia matumaini.