2014-06-18 09:02:38

Mwanamke apeta kwa mara ya kwanza Tuzo la Ratzinger, 2014


Mfuko wa Josefu Ratzinger, Benedikto XVI kwa mwaka 2014 umetoa tuzo kwa mara ya kwanza kwa mwanamke Anne-Marie Pelletier anayefundisha Maandiko Mtakatifu, kutoka Ufaransa pamoja na Monsinyo Waldermar Chrostowski, mtaalam wa Maandiko Matakatifu, kutoka Poland. Washindi hawa watatunukiwa tuzo yao katika maadhimisho ya tuzo hii kwa awamu ya nne hapo tarehe 22 Novemba 2014.

Tuzo hii itakwenda sanjari na maadhimisho ya kongamano la kimataifa litakaloongozwa na kauli mbiu "heshima kwa zawadi ya uhai, hija ya imani" na kufanyika Chuo kikuu cha Kipapa cha Medellin, kilichoko nchini Colombia. Hayo yametangazwa na Kardinali Camillo Ruin pamoja na viongozi waandamizi kutoka katika Mfuko wa Josefu Ratzinger, Benedikto XVI wakati walipokuwa wanazungumza na waandishi wa vyombo vya habari mjini Vatican, Jumanne, tarehe 17 Juni 2014. .

Mama Anne- Marie Pelletier ni mwanamke ambaye amejipambanua kwa kuandika kuhusu dhamana na wajibu wa wanawake katika Ukristo na Kanisa kwa ujumla. Ni vitabu ambavyo vinafafanua kwa kina na mapana mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Ruini anasema kwa hakika Mama Anne-Marie ni mwanamke wa shoka anayejipambanua kutokana na weledi wake katika kuyachambua Maandiko Matakatifu kwa kuonesha mchango na ushuhuda wa wanawake Wakristo katika maisha ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Monsinyo Waldermar Chrostowski ni mhariri mkuu wa Jarida la Kitaalimungu linalochapishwa nchini Poland lijulikanalo kama "Collectanea Theologica". Kuanzia mwaka 2004 ni Rais wa Chama cha Wataalam wa Maandiko Matakatifu nchini Poland. Ni mwandishi na mtaalam ambaye anaendelea kuwashangaza wengi kutokana na ufundi mkubwa anaoutumia katika kuchambua Maandiko Matakatifu. Ni mwandishi aliyebobea kiasi kwamba anaendelea kuchangia kwa dhati kabisa katika ufahamu wa Maandiko Matakatifu na mchakato wa majadiliano kati ya Wakristo na Wayahudi. Ni Jaalimu pia wa Maandiko Matakatifu.

Katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Josefu Ratzinger, Benedikto XVI, kazi zake zimeendelea kupanuka kiasi kwamba, leo hii kuna vyuo vikuu 275 kutoka sehemu mbali mbali za dunia vinavyofanya tafiti mbali mbali, kwa kuwahusisha majaalimu na wanafunzi 1600. Kumbe, maadhimisho ya Kongamano la Mfuko wa Josefu Raztinger, kuanzia tarehe 23- 24 Oktoba, 2014 ni mwendelezo wa juhudi hizi katika ngazi mbali mbali za kimataifa







All the contents on this site are copyrighted ©.