2014-06-18 11:57:44

Kenya inalilia amani na utulivu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitishwa sana na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza nchini humo kiasi cha kuwanyima wananchi amani na utulivu. Zaidi ya watu 50 wamepoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa hivi karibuni katika eneo la Mpeketoni, kiasi cha kuwaacha wananchi wakiwa na maswali magumu yasiyokuwa na majibu! Vyombo vya ulinzi na usalama viko wapi wakati wa mashambulizi kama haya?

Wananchi wa Kenya wanakumbushwa kwamba, ulinzi na usalama wa Kenya uko mikononi mwa wananchi wenyewe, kumbe ni jukumu lao kuwa macho kila wakati. Usalama unaweza kupatikana wanasema Maaskofu ikiwa kama utawala wa sheria utazingatiwa na watu wataheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi. Jambo la msingi ni kila mwananchi kulinda na kutetea zawadi ya uhai, utu na heshima ya binadamu, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Tume ya haki na amani na kutiwa sahihi na Askofu mkuu Zaccheus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya unasema kwamba, hali ya kisiasa nchini Kenya ni tete kiasi kwamba inaatishia mustakabali wa taifa, amani na utulivu. Kuna haja ya kuangalia tena kwa umakini mkubwa kuhusu Kipengele cha 33 cha Katiba kuhusu uhuru wa mtu kujieleza, jambo ambalo halina budi kuwashirikisha wadau mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wengi.

Hali ya kisiasa na kijamii nchini Kenya ni tete kiasi kwamba, kuna wasi wasi wa kuibuka tena kwa machafuko ya kisiasa kama yale yaliyojitokeza mara tu baada ya uchaguzi mkuu nchini humo kunako mwaka 2007. Kuna changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza nchini Kenya kwa mfano: idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha nchini humo, rushwa na ufisadi wa mali ya umma, kinzani za kikabila, ukosefu wa amani na utulivu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linashauri Serikali na wadau mbali mbali kubainisha sera makini za ulinzi na usalama kwa ajili ya wananchi wa Kenya; kuimarisha intelijensia ya kitaifa ili kudhibiti vitendo vya kigaidi, utawala wa sheria kushika mkondo wake, kufanya marekebisho makubwa kwenye Jeshi la Polisi pamoja na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu masuala ambayo yamepelekea Kenya kuyumba na hivyo kusababisha machafuko ya kijamii.

Kumbe, ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana, umaskini, umiliki wa ardhi pamoja na kuponya madonda ya chuki za kikabila ambazo zimekuwepo nchini Kenya kwa miaka mingi, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Wakenya watafute mafao ya wengi kwa kujikita katika ustawi na maendeleo ya Wakenya wote, ili kuondoa "ndago" za Ukabila zinazoendelea kuwatesa wengi. Kanisa liko tayari kusaidia mchakato wa kupatikana kwa mustakabali wa taifa la Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.