2014-06-18 14:07:00

Kanisa ni Mama, Familia na Fumbo linalowakumbatia binadamu wote!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza mzunguko wa Katekesi Mpya, Jumatano tarehe 18 Juni 2014 kwa kutafakari kuhusu Kanisa, lakini kabla ya Katekesi yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwatembelea na kuwasalimia wagonjwa na wazee waliokuwa wanafuatlia Katekesi yake kwenye Ukumbi wa mikutano wa Paulo VI. Roma kwa sasa jua linawaka bila utani na wakati mwingine linaambatana na mvua kubwa!

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa si tu kwamba inatambulika kama taasisi, bali pia ni Mama, ni Familia na Fumbo linalowakumbatia binadamu wote. Kanisa lilianzishwa na Yesu Kristo lakini historia yake inayojionesha tangu wakati wa Agano la Kale, wakati ule Mwenyezi Mungu alipomwita Abrahamu kutoka katika nchi yake na kuelekea kwenye Nchi ya ahadi na kwamba, angefanywa kuwa ni Baba wa taifa kubwa na baraka kwa watu wa mataifa.

Hii ina maana kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayepiga hatua ya kwanza: akamchagua Abrahamu na watu wa nyumbani kwake kumfuasa katika hija ya imani. Si kila wakati njia anayoitumia Mwenyezi Mungu inaweza kufahamika mara moja, kwani wakati mwingine inasheheni vikwazo, majaribu pamoja na kukosa uaminifu.

Historia ya Watu wa Mungu, yaani Kanisa ni kielelezo cha uaminifu wa Mungu unaojikita katika huruma na upendo usiokuwa na kifani. Ni kutokana na msaada wake, waamini wanaweza kushinda dhambi zao na kuendelea kudumu katika njia iliyooneshwa kwao na Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Yesu alienzi Kanisa lake katika hija ya imani katika historia na kuwaongoza waamini kwenye njia iendayo mbinguni pamoja na kufanya baraka zake ziwe ni alama ya upendo wa Mungu kwa watoto wake.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kanisa ili waweze kuwa kweli ni alama ya upendo wa Mungu kwa watu wote. Wakumbuke daima kwamba, kila wakati wanaposoma na kulitafakari Neno la Mungu, wanaisikiliza sauti ya Yesu, mwaliko wa kutoka katika ulimwengu wao mdogo, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, unaomkirimia mwanadamu uhuru wa kweli.

Anawashauri waamini kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwafunda na hatimaye wawe ni baraka kwa wengine kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha mahujaji kwamba, Kanisa linasherehekea Jubilee ya miaka 75 tangu Papa Pio XII alipowatangaza Mtakatifu Francisko wa Assis na Katarina wa Sienna kuwa ni wasimamizi watakatifu wa Italia. Katika mkesha wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu ambayo kwa majimbo mengi itaadhimishwa Jumapili ijayo. Lakini, Alhamisi tarehe 19 Juni 2014 mjini Vatican, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na baadaye kuongoza maandamano ya Ekaristi Takatifu kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujichotea nguvu itakayoimarisha imani yao kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Wagonjwa waendelee kumwabudu Yesu wa Ekaristi katika shida na mahangaiko yao ya ndani na wanandoa, wachote upendo wao wa dhati kutoka kwa Kristo aliyejisadaka kwa ajili ya binadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.