2014-06-18 09:33:27

Jubilee ya miaka 500 ya Jimbo Katoliki Funchal, Ureno


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, hivi karibuni kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Jimbo Katoliki la Funchal kama kilele cha Jubilee ya miaka mia tano tangu kuzinduliwa kwa Jimbo hili ambalo liko huko Madeira nchini Ureno.

Kardinali Filoni anasema, hiki ni kipindi cha kujikita zaidi na zaidi katika ari na maisha ya kimissionari, tayari kwenda kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha.

Ibada hii imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali bila kuisahau Familia ya Mungu nchini Ureno. Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amekazia umuhimu wa upendo miongoni mwa Watu wa Mungu, ili uwawajibishe kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa ndani na nje ya nchi yao. Waamini wajitahidi kuwaonjesha wale ambao wako mbali na Kanisa, ili kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 500 ya Jimbo Katoliki Funchal yalianza kunako mwaka 2011 hadi mwaka 2014, kwa kukazia umuhimu wa Kanisa kujipambanua zaidi katika kazi za kimissionari, ili kuwawezesha waamini kuendelea kuwa hai na kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha waamini kujikita katika utume wa kimissionari, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha kwa kuwashirikisha jirani zao imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Filoni amewashukuru na kuwapongeza waamini wa Jimbo Katoliki Funchal kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia; tangu Afrika, Amerika ya Kusini na India. Huu ni ushuhuda makini wa Jumuiya ya Kikristo inayothamini umuhimu wa Uinjilishaji pamoja na kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Haya ndiyo maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.