2014-06-18 08:21:49

Dini na mchakato wa maendeleo ya kweli!


Kanisa linaendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Yohane Paulo II katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Ni kiongozi anayekumbukwa kutokana na mchango wake uliosaidia kuanguka kwa ukomunisti Ulaya Mashariki, miaka ishirini na mitano iliyopita, tukio ambalo limeleta mabadiliko makubwa na changamoto nyingi. RealAudioMP3

Kunako mwaka 1989 Mtakatifu Yohane Paulo II alichapisha Waraka unaojulikana kama “Annus Mirabilis”. Poland kwa mara ya kwanza ikafanya uchaguzi huru na hatimaye, kuanguka kwa Ukomunisti Ulaya Mashariki.

Hivi karibuni Ubalozi wa Poland mjini Vatican kwa kushirikiana na Taasisi za Kipapa za Sayansi waliadhimisha tukio hili ambalo liliwashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa kutoka mjini Vatican na Poland. Baadhi ya wadau wakuu katika mageuzi haya kama vile Lech Walesa, Rais mstaafu wa Poland alitoa ushuhuda wake na kuwataka wananchi wa Poland kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa siku za usoni, kwa kuzingatia amri kumi za Mungu, msingi mkuu wa maadili na utu wema.

Jamii haina budi kujikita katika urithishaji wa tunu msingi za maisha ya kijamii, ili kujenga jamii inayowajibika na kujikita katika maadili mema. Wadau mbali mbali wametambua mchango uliotolewa na Kanisa katika kuanguka kwa utawala wa kikomunisti Ulaya Mashariki hata kama Kanisa liliteseka na kudhulimiwa sana katika nyakati hizi.

Waamini walei kwa njia ya ushuhuda makini wa maisha yao, walijielekeza zaidi na zaidi katika kuleta mabadiliko, leo hii Ulaya ya Mashariki licha ya magumu na changamoto nyingi, lakini imeshuhudia mabadiliko ya kweli, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa mawasiliano. Majadiliano kati ya watu wasioamini na waamini walei yanayofanyika katika uhalisia wa maisha ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato unaopania kuyatakatifuza malimwengu. Bila kanuni msingi za maadili na utu wema, dunia inakuwa ni uwanja wa fujo.

Kardinali Paul Poupard, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, Kanisa lilikuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa kuwajengea watu msingi bora wa maisha ya kiroho dhidi ya ukanimungu pamoja na kuendelea kuimarishwa kwa mfano na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyekuwa chemchemi ya imani na matumaini kwa wananchi wengi wa Ulaya ya Mashariki. Kwa njia hii, watu wengi wakaweza kupata uhuru wa ndani ambao matunda yake yalijionesha kwa nje katika masuala ya kisiasa na kijamii.

Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ambaye aliwahi kuwa Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, Vatican kuanzia kwenye uongozi wa Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI ilijihusisha kikamilifu katika kuwajengea watu uwezo wa kujiletea mabadiliko ya kweli katika maisha yao, kwa kuunga mkono uhuru wa kidini na haki msingi za binadamu. Mambo yote haya yanaonesha nguvu ya kidini na imani katika mchakato wa kumletea mwanadamu ukombozi wa kweli. Kwa njia ya nguvu ya imani, mataifa yanaweza pia kupata amani ya kweli kwa siku za usoni!








All the contents on this site are copyrighted ©.