Mafisadi wanaangamiza maisha ya watu, njia pekee ni kutubu!
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha,
Jumanne, tarehe 17 Juni 2014 anasema: rushwa, ufisadi, mauaji na nyanyaso dhidi ya
wanyonge kama ambavyo Mfalme Ahabu wa Israeli alivyomtenda Nabothi ni mambo yanayomkasirisha
sana Mwenyezi Mungu na mwaliko kwa watu kama hawa ni kutubu dhambi zao ili kuonja
tena huruma na upendo wa Mungu, vinginevyo hasira ya Mungu itawaka juu yao!
Mafisadi
wa aina zote ni watu ambao wanawafanya watu wa Mungu kutenda dhambi na hivyo kumkasirisha
Mwenyezi Mungu. Yesu katika mafundisho yake anaonya watu ambao wanakuwa ni kikwazo
kwa Jamii, kuwa makini kwani wanaweza kuonja hasira ya Mungu kama inavyojionesha kwenye
Liturujia ya Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha kwanza cha Wafalme, Sura ya 21:17
- 29.
Lakini pia Baba Mtakatifu anaonya kwamba, kama mtu hana uhakika kuhusu
ufisadi na vitendo vya rushwa au mauaji yaliyofanywa na mtu ni vyema kukaa kimya kwani
kumhukumu kwamba, ni fisadi ni sawa na kumwondosha machoni pa Mungu. Kwa wale wanaoiba,
wanaoua na kuwanyanyasa maskini, watakiona cha mtema kumi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Mfalme Ahabu aliposikia hasira ya Mungu imemwakia, alitubu na kujinyenyekesha
mbele ya Mungu kwa kuomba msamaha wa dhambi zake. Hii ndiyo njia mafisadi ndani na
nje ya Kanisa wanapaswa kuifuata, kama alivyofanya Zakayo Mtoza ushuru aliyekutana
na Yesu akatubu na kuongoka, akarudisha mali aliyokuwa ameiba na hivyo kuanza maisha
mapya.
Kwa mafisadi, wala rushwa na wauaji wasiotubu watakufa wakiwa wameelemewa
na dhambi zao mioyoni mwao. Watu wana haki ya kulaani na kuwashutumu mafisadi, lakini
pia wawe na ujasiri wa kuomba neema kutoka kwa Mungu ili nao wasitumbukie katika mtindo
huo wa maisha, na hatimaye, wakakiona cha mtema kuni mbele ya Mwenyezi Mungu!