2014-06-16 07:01:08

Shule ya Yesu ni kiboko!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani. Tumsifu Yesu Kristo! Baada ya kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu kwa adhimisho la Sherehe ya Pentekoste, sasa tuendelee kuyarutubisha maisha yetu ya imani kwa mwanga wa fadhila za Moyo Mtakatifu wa Yesu. RealAudioMP3 RealAudioMP3

Tunafanya hivyo tukijua kuwa huu ni mwezi JUNI ambapo kadiri ya desturi zetu Katoliki, tunauheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni upendo wa Yesu, upendo usio na kikomo ndio uliomsukuma afanye yote aliyofanya kwa ajili yetu. Alikuja duniani, alihubiria watu ufalme wa Mungu, aliponya wagonjwa, alifufua wafu, aliwapa nafuu ya roho waliolemewa na mizigo mizito ya dhambi na mwisho akatoa sadaka ya uhai wake kwa njia ya mateso na kifo chake msalabani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.

Kristo Yesu, anapenda sisi sote tujifunze na tuige upendo wake. Ni kwa njia hiyo, tutaweza kusali kama alivosali yeye, kufundisha kama alivyofundisha yeye, kuhurumia na kuhudumia wagonjwa kama alivyofanya yeye, kuwatetea wanyonge na kuwainua waliopondeka moyo kama alivyofanya yeye. Yeye mwenyewe katika neno lake anatualika akisema “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mt. 11:29-30).

Yesu anapotualika tujifunze kwake, maana yake anapenda tuishi kadiri alivyotufundisha yeye aliye mwema na mkamilifu. Ndio maana tunatafakari juu ya Shule ya Yesu. Katika shule ya Yesu, ambamo Kristo mwenyewe ndiye Bwana na Mwalimu tunajifunza mambo mengi sana. Machache yake ni haya:-

Utii
Utii ni fadhila inayotudai kuwa tayari kutekeleza kwa uaminifu matakwa sahihi ya wakubwa wetu (kama ni katika familia wazazi na walezi wetu, kama ni shuleni kuwatii walimu, katika Kanisa kuwatii viongozi wetu wa Kanisa, na katika serikali kutii mamlaka HALALI na MIONGOZO SAHIHI ya viongozi wetu). Utii ni fadhila ngumu kuliko zote kwani hudai kuusadaka uhuru na utashi wako na kujisalimisha kwa matakwa ya mtu mwingine. Na hapo ndipo penye kipimo cha Ukomavu. Mtu mkomavu huonekana katika kutii kwake. Na kinyume cha Utii ni KIBURI-kikavu.

Injili zinatushuhudia jinsi Yesu alivyokuwa na utii kwa wazazi wake, na zaidi ya hayo alikuwa mtii hata mauti. Aliyapokea yote kwa sababu alitii mapenzi ya Mungu baba yake. Na kwa sababu hiyo ametuletea ukombozi.

Katika familia zetu, endapo tangu mwanzo tunafundishana UTII basi tunaunda watu wema wenye kujenga ufalme wa amani duniani. Familia isiyojua utii, kila mtu anakuwa mjuaji na msemaji mkuu (baba mjuaji, mama mjuaji, watoto ni wajuaji hakuna mfano, hakuna anayemsikiliza wala kumtii mwenzake), matokeo yake hakuna masikilizano na mwishowe ni kelele, fujo na matusi na mapigano yasiyokoma. Utii hujenga unyamavu na unyamavu hufungua mlango wa masikilizano mema, na hapo ndipo kama familia sote kwa pamoja twaweza kujenga maendeleo ya familia na kumjenga kila mmoja wetu kuwa mtu wa kufaa.

Unyenyekevu
Katika shule ya Yesu tunajifunza unyenyekevu. Ndiyo maana tunasali daima tukisema, ‘Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako’. Unyenyekevu ni fadhila inayotualika kutotafuta makuu. Ni fadhila inayotualika kuwaona wengine kuwa bora zaidi kuliko sisi, (Fil. 2:3-4), ni fadhila inayotualika kujishusha zaidi kuliko kupenda kujikweza na kujitutumua-tutumua.

Ni katika unyenyekevu tunatambua na kujikubali kasoro zetu, ni katika unyenyekevu pia tunakubali karama zetu na za wengine, na pia tunaheshimu kasoro zao, na kusahihishana kwa upendo inapowezekana, ikishindikana tuvumiliane bila matangazo.

Tukikosa fandhila ya unyenyekevu, daima tutajiona kuwa sisi ndio wenye haki, na daima tutatafuta haki na sifa zetu, na wakati huohuo tutakuwa tunakanyaga pua za wengine, ili sisi tutukuzwe. Unyenyekevu hutusaidia kutenda haki na kuishi kwa haki.

Tukikosa unyenyekevu, tunatesa wenzetu bila sababu. Usipokuwa mnyenyekevu, makosa yako utawasingizia wenzako, hata dhambi zako binafsi utadhani zinasababishwa na wenzako. Utaharibu kazi za ofisi na za umma, na hutaki kukubali kuwa huwezi. Katika mazingira yetu ya kazi za pamoja, mfanyakazi asiye mnyenyekevu, ni mzigo na kero kubwa kwa wenzake, hata kama anafanya mazuri. Unyenyekevu huyapamba matendo yetu mema, hata kama ni madogo, yataonekana makubwa sana kama tunayatenda kwa unyenyekevu. Lakini hata kama ukafanya mambo makubwa vipi, yasiyo na unyenyekevu, hayo yanakuwa na harufu mbaya tu.

Upole
Katika shule ya Yesu tunajifunza upole. Kristo Yesu alikuwa mpole. Fadhila ya upole hujengwa na utulivu wa akili, utulivu wa nafsi na utulivu wa maisha. Tusipokuwa wapole, ndani tunajenga sumu ya ukorofi na sumu ya roho mbaya, inayotufanya daima tuwachukie watu kwa chukio kamili la kiapo, na mwisho tunaishia kuhisi kuwa hatupendwi. Upole sio uzubavu, na wala sio unyonge, bali ni uungwana.

Yoshua bin Sira anasema “Mwanangu, uwe mpoke katika shughuli zako, nawe utapendwa na wale wanaokubaliwa na Mungu” (Ybs. 3:17), na pengine anasema “maneno ya upole humwongezea mtu marafiki, kuongea kwa upole husababisha hisani” (6:5), na pengine aonya akisema, “usiwe kama simba nyumbani mwako, wala mwenye kupenda kuwafokea na kuwatuhumu watumishi wako” (4:30). Upole, ni daraja ya kufikika na watu wengi. Ukikosa upole utafukuza hata wanyama.

Imani na sala
Shule ya Yesu ni shule ya imani na sala. Maisha ya Yesu yalipambwa kwa sala daima. Anatuelekeza daima tusali akisema, “kesheni mkiomba msije mkatiwa majaribuni” Mt.26:41. Na pengine asema “Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa”. . Na sisi tunataka kwa dhati kabisa tujenge roho ya kujifunza kusali na kupenda kusali.

Tumwinulie Mungu mioyo yetu kwa sala nyakati zote. Tusisubiri tu tukizabuliwa na matatizo. Na kwa kweli, sala ni mafuta yanayolainisha mahusiano yetu na Mungu na mahusiano yetu na wenzetu.

Basi, mpendwa msikilizaji, tukiwa ndani ya mwezi huu tunapouheshimu kwa namna ya pekee kabisa Moyo Mtakatifu wa Yesu, tuendelee kujiweka wakfu kwake, ili mioyo yetu ifanane na moyo wake. Tunapenda kutumia nafasi hii kutoa hamasa ya kichungaji kwa waamini wote, tupende kujiunga na vyama vya kitume katika kanisa. Ukitaka kufahamu vizuri SIRI KUU ya Moyo wa Yesu, jiunge na USHIRIKA wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, jiweke miguuni pake, sikiliza neno lake, tega sikio sikiliza siri za moyo wake, hakika muumini mpendwa, utapata faraja, amani na pumziko jema.

Tunapoendelea kujifunza katika shule ya Yesu, tusali sote tukisema “Ee Yesu mwenye Moyo mpole na mnyenyekevu, ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako”. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.