2014-06-16 09:34:48

Papa Francisko kutembelea Albania nchi ya mashahidi wa imani!


Taarifa ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Albania hapo tarehe 21 Septemba 2014 imepokelewa kwa furaha na bashasha na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema nchini Albania. Hii itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Albania, lakini pia atapata nafasi ya kukutana na kusalimiana na wananchi wa Albania katika ujumla wao.

Askofu mkuu Ramiro Molinar Ingles, Balozi wa Vatican nchini Albania anasema, mwaliko kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Albania ulitolewa na viongozi wa Kanisa na Serikali nchini Albania, wakati Waziri mkuu wa Albania Bwana Edi Rama alipotembelea Vatican mwezi Aprili, 2014. Hii itakuwa ni hija ya kwanza ya kitume kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika nchi za Ulaya.

Baba Mtakatifu anatembelea Albania kama nchi ambamo Wakristo wengi wanajisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na damu yao imekuwa ni chemchemi ya kukua na kuenea kwa Injili. Atatembelea Albania mahali ambako majadiliano ya kidini na kiekumene yanaendelea katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu atatembelea Albania kwa siku moja, lakini hata hii inatosha kuwaimarisha ndugu zake katika imani na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake







All the contents on this site are copyrighted ©.