2014-06-16 09:31:20

Papa aguswa na mateso ya wananchi wa Iraq!


Mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 16 Juni 2014, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake nchini Iraq ambako machafuko ya kisiasa yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hadi sasa kuna watu wengi waliopoteza maisha na kati yao kuna Wakristo ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwahakikishia wananchi wote wa Iraq uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli amani, utulivu na upatanisho wa kweli viweze tena kupata nafasi katika mioyo ya wananchi wa Iraq kwa ujumla wao! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa njia ya sala ili kuwaombea wananchi wa Iraq katika kipindi hiki kigumu cha historia ya nchi yao.

Baba Mtakatifu ametangaza pia kuwa tarehe 21 Septemba 2014 anatarajia kutembelea nchi ya Albania ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani na mapendo, ili waweze kushuhudia tunu hizi katika maisha yao. Anasema, Albania ni nchi ambayo imeteseka sana kutokana na kinzani na migogoro ya kisiasa.

Baba Mtakatifu amewataka wanachama wa Chama cha kuhamasisha utakatifu wa maisha, kutekeleza dhamana hii kwa furaha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee watumishi wa nyumbani ambao wanafanya kazi nzuri sana kwa familia, hasa kwa kuwasaidia wazee na watu wasiojiweza. Lakini kwa bahati mbaya, hawathaminiwi na wakati mwingine wananyimwa haki zao. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa moyo wa dhati kabisa!







All the contents on this site are copyrighted ©.