Sherehe za Fumbo la Utatu Mtakatifu ni mwaliko kwa waamini kutafakari na kumwabudu
Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, wanaonesha maisha ya umoja na upendo mkamilifu,
chanzo na kilele cha viumbe vyote. Kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanapata
fursa ya kutambua muundo wa Kanisa ambalo waamini wanaalikwa kulipenda kama Yesu mwenyewe
alivyowapenda upeo! Ni upendo unaonesha imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Hii
ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika
wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe
15 Juni 2014 wakati wa Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anasema, upendo ni kielelezo
makini cha Ukristo unaonesha urafiki wao na Yesu Kristo. Chuki, kinzani na uhasama
ni mambo ambayo kimsingi yanapinga na Ukristo kwani Mungu ni upendo.
Waamini
wote wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia kwamba, Mungu ni upendo
na anafanya hija na watu wake katika shida na mahangaiko yao; katika furaha na raha.
Mwenyezi Mungu ameupenda hivi ulimwengu hata akatwaa mwili na kufanyika mwanadamu,
ili aweze kuukomboa ulimwengu kwa njia ya Yesu Kristo. Huu ndio ule upendo unamwezesha
Mwenyezi Mungu kusamehe na kwa njia ya Yesu Kristo, waamini wanaonja upendo wa Mungu.
Roho
Mtakatifu ni zawadi ya Yesu Kristo Mfufuka, anayewakirimia waja wake maisha mapya
na kuwawezesha kushiriki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, katika upendo, umoja, huduma
makini na kushirikishana. Mtu anayependa kwa sababu ya upendo wenyewe anaonesha ile
taswira ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hivi ndivyo ilivyo pia kwa familia na kwa parokia
katika ujumla wake, kwani watu wanapopendana na kushirikishana mambo ya kiroho na
kimwili, wanaonesha ile taswira ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Baba Mtakatifu
anasema, huu ni upendo usiokuwa na mipaka, upendo unaoheshimu uhuru wa wengine na
kwamba, kila Jumapili, waamini wanaadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo
cha moto wa upendo, hapa linaishi Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ndio maana Kanisa
linaadhimisha Siku kuu ya Ekaristi Takatifu mara baada ya kuadhimisha Fumbo la Utatu
Mtakatifu.
Alhamisi, ijayo, tarehe 19 Juni 2014 Baba Mtakatifu Francisko anasema
anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kufanya maandamano ya Ekaristi
Takatifu kutoka kwenye Kanisa kuu la Yohane wa Laterano hadi kwenye Kanisa kuu la
Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Anawaalika waamini na mahujaji kushiriki kwa
wingi katika tukio hili la imani.