2014-06-16 07:22:48

Mshikamano wa Kanisa kwa wananchi wa Iraq


Kardinali Leonardo Sandri, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki akiungana pamoja na wakuu wa Mashirika na wafanyakazi wa Baraza hili anapenda kuonesha mshikamano wa dhati na Patriaki Luis Sako wa Kanisa la Wakaldei wa Babilonia, tangu kuchaguliwa kwake amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, waamini wa Makanisa mbali mbali wanajikita katika mchakato wa majadiliano na upatanisho wa kitaifa.

Kwa namna ya pekee, Baraza la Kipapa linapenda kuonesha pia mshikamano wake kwa wananchi wa Iraq wanaokabiliana na machafuko ya kisiasa ambayo yamepelekea maelfu ya watu kuyakimbia makazi ili kuyasalimisha maisha yao, kiasi cha kusababisha maafa na usumbufu mkubwa. Makanisa na Taasisi zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Iraq ziko wazi kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi. Kanisa linashirikiana na viongozi wengine wa dini kuwasaidia wakimbizi hawa kwa hali na mali.

Ni matumaini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kwamba, Sala ya kuombea amani Mashariki ya Kati wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, itazaa matunda kwa wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati.








All the contents on this site are copyrighted ©.