2014-06-16 09:39:43

Kumhudumia maskini ni kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu!


Professa Andrea Riccardi mwanzilishi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma wakati akitoa hotuba ya makaribisho kwa Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Jumuiya hiyo, Jumapili tarehe 15 Juni 2014 anasema, ni ndoto ya Jumuiya yake kuwa ni Kanisa kwa ajili ya wote, lakini zaidi kwa kutoa kipaumbele kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Wanataka kuchangia katika mchakato wa mabadiliko duniani kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Yesu na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanataka kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, muujiza ambao unawezekana kwa njia ya imani, sala na majadiliano ya kweli. Kwa hakika anasema Professa Riccardi inapendeza kuwa Mkristo.

Baba Mtakatifu akiwa kwenye Kanisa la Bikira Maria wa Trastevere mjini Roma alipata nafasi ya kusikiliza shuhuda zilizotolewa na watu wanane wanaowakilisha makundi ya wale wanaohudumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yaani: Wazee, wakimbizi, maskini, walemavu na watu wasiokuwa na fursa ya ajira.

Askofu mkuu Jean Kawak wa Kanisa la Kiorthodox, Jimbo kuu la Damasko anasema kuna viongozi mbali mbali wa kidini wametekwa nyara nchini Syria na wanaendelea kuteseka na kwamba, Kanisa linasubiri kwa imani na matumaini siku ambayo wataachiliwa huru. Wananchi wa Syria wanateseka kutokana na baa la njaa, magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira na umaskini. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 160, 000 wamefariki dunia katika vita inayoendelea nchini Syria. Pamoja na changamoto zote hizi watu bado wana imani na matumaini ya Syria bora zaidi.

Bibi Irma Lombardi, mwenye umri wa miaka 90 amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha upendo pamoja na kuwajali wazee kinyume kabisa cha utamaduni unaoendelea kujengeka kwa sasa wa kutowathamini wala kuwajali wazee. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa muda wa miaka 20 imemsaidia kuonja upendo na ukarimu wa Familia ya Mungu na kwamba, kuwa mzee si dhambi bali ni sehemu ya mchakato wa maisha. Kanisa lijenge utamaduni wa kuwasaidia na kuwahudumia wazee hasa katika maisha yao ya kiroho. Kuwasaidia maskini ni kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu.

Vijana wanasema wao wanapenda kushiriki katika Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ili kudumisha misingi ya haki na amani, kwa kuwasaidia na kuwahudumia wazee na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kutambua na kuthamini utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kwa kusaidiana kuwawawezesha watu kupata chemchemi ya maisha.

Baadhi ya watu wasiokuwa na fursa za ajira wanasema, wana familia na watoto, wanakosa furaha ya kweli kwa vile hawana ajira na fedha za kuweza kuhudumia familia zao. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimepelekea watu wengi kukosa ajira kiasi kwamba, utu wao umewekwa rehani.

Baadhi ya watu katika ushuhuda wao wanasema, maisha yao yamebadilika kwa haraka baada ya kuwapoteza wazazi, wenzi na wapendwa wao. Lakini kwa njia ya marafiki wema na watakatifu wameweza kuwasaidia kuonje furaha na matumaini tena katika maisha, kiasi kwamba, hata wao wanapenda kuwahudumia wengine kama alama ya shukrani. Hakuna furaha kubwa kama kujenga urafiki na Yesu, kwa kusikiliza Neno pamoja na kushiriki Sakramenti za Kanisa. Leo hii wanayo furaha ya kuwatangazia wengine Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa huduma!

Baadhi ya watu wanaohudumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio mjini Roma wanasema, kutokana vita, dhuluma na kinzani za kijamii wamelazimika kuzikimbia nchi zao na sasa wanaishi katika mazihngira hatarishi, lakini wameona mwanga wa amani na utulivu kutoka katika Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta na hatimaye kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la Zingari wanaolazimika kuishi mafichoni na hivyo kuendelea kunyanyasika na kwamba, hata wao wanawajibika kuwa wajenzi wa haki na amani katika Jamii inayowapatia hifadhi.

Baadhi ya wakimbizi wanasema, wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita na dhuluma za kikabila, ambazo zinawafanya wakati mwingine kuamua kuchukua maamuzi magumu katika maisha. Safari ya kutafuta maisha bora ughaibuni ina gharama na magumu yake; ina hatari na hasara zake; daima kifo kiko mkononi! Ameshuhudia baadhi ya rafiki zake wakifa maji bila msaada wowote ule. Ni safari ya hatari, chini ya uvungu wa gari kwa muda wa masaa 35! Baadhi ya vijana wanashindwa kuvumilia na hivyo wanajikuta wakianguka barabarani na kugongwa na magari! Hata wakimbizi na wahamiaji wanatamani kuona amani na utulivu vikitawala nchini mwao!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.