Mwenyezi Mungu ameongea nasi katika historia. Hivyo hata hii sherehe ya leo ni matokeo
ya uwepo huo wa Mungu katika matukio ya maisha yetu. Mungu amejionesha katika matukio
ya maisha ya mwanadamu. Katika somo la kwanza – halizungumzii Utatu Mtakatifu - ila
zipo dalili za ukweli huo. Iko wazi habari ya Mungu mmoja wa Israel - Mungu ni mmoja.
Na huyu Mungu anaonekana kwao katika matukio mbalimbali ya maisha yao ambayo kabla
yake hayakuwa hivyo.
Katika somo la Pili – Mtakatifu Paulo anaonesha Utatu
ukiwa kazini - hatuna maelezo ya utatu mtakatifu yanayotolewa - bali ni nini Mungu
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanafanya katika maisha yetu. Aongea juu ya ua na n.k
ila hilo linawezekana kwa sababu ya ufunuo wa Mwana na kwa njia yake sisi tunakuwa
waana.
Je, Mtume Paulo alifahamuje ukweli huu?Ni katika maisha ya wafuasi
na katika maisha yake mwenyewe. Wote walimwita Mungu Baba kama alivyofanya Yesu. Ni
nguvu gani inamsukuma Paulo? Ni roho wa Mungu. Katika barua nyingine za mtume Paulo
aongea kumtambua roho katika nafasi mbalimbali kama kufundisha kuponya n.k.
Katika
somo la Injili – habari juu la Fumbo la Utatu Mtakatifu iko wazi. Mitume na wafuasi
wanatumwa kubatiza na katika ubatizo fumbo la Utatu Mtakatifu huanza kuwepo katika
maisha yetu. Ungamo la imani yetu huthibitisha rasmi tamko letu la upendo kwa fumbo
hilo.
Mtakatifu Agostino wa Hippo akitaka kueleza utatu mtakatifu kadiri ya
akili ya mwandamu - siku moja akitafakari jambo hili maeneo ya ufukweni ghafla akamwona
mtoto mdogo peke yake ufukweni. Huyo mtoto alikuwa ametengeneza kishimo na alikuwa
akichota maji baharini na kuyamwaga katika kale kashimo.
Mtakatifu Agostino
akamwuliza unafanya nini? Mtoto akamjibu nataka kuweka bahari hii katika kashimo haka.
Mt. Agostino akamwambia itawezekanaje? Kujaza kashimo haka kwa maji ya bahari yaliyo
mengi kiasi hiki? Naye yule mtoto akamwambia nawe je wadhani kuwa kichwa chako kidogo
na moyo wako mdogo utaweza kuelewa kwa kina na kupenda kikamilifu fumbo la utatu mtakatifu?
Mara mtoto yule akatoweka.
Rom 5.1-5 huunganisha utatu mtakatifu na maisha
ya kila siku ya mkristo. Mtakatifu Paulo anaunganisha mtandao mzima wa haki na wokovu
kama kuwa na amani na Mungu. Kuwa na uhusiano na Mungu ni wajibu wetu mkuu na ni njia
ya Kristo - 5:1-2 - basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani na tuwe na
amani kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia
ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake katika tumaini la utukufu
wa Mungu.
Lengo letu ni kuwa pamoja na Baba. Hii inawezekana kwa njia ya Kristo.
Matumaini yetu ni kushiriki utukufu wa Mungu. Hii huwezekana kwa njia ya imani inayotupa
matumaini. Mungu ametupa matumaini hayo - 5:5 na tumaini halihatarishi kwa maana pendo
la Mungu limekwisha kumininwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.
Huu upendo wa Mungu umemwagwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Msingi
wa maisha ya Kristo hujengwa katika Utatu Mtakatifu na hii ndiyo tofauti moja kubwa
kati ya dini ya kikristo na dini nyingine. Dini nyingine hutazama mhusika (mwamini)
na Mungu wake tu. Ukristo pia una mtazamo huo, ila huongeza uwepo wa Yesu kristo anayetuunganisha
na Baba na Roho Mtakatifu anayetutakatifuza. Wajibu wetu wa kikristo hauanzii na kuishiatu
katika imani kwa Kristo na kupewa haki na Mungu. Huo tu ni mwanzo toka hapa huanza
kazi ya kusaka wokovu, kuwa watakatifu kama baba alivyo mtakatifu.
Sherehe
ya PENTEKOSTE tuliyosherekea jumapili iliyopita inashika kasi hapa. Kwa njia ya roho
upendo wa Mungu humwaga mioyo mwetu na kwa njia yake tunajifunza kumpenda Mungu na
jirani kama alivyotufundisha Bwana. Swali muhimu - hili fumbo linatuambia nini
juu ya Mungu tumwaminiye na ni aina gani ya watu tunapaswa kuwa? Mambo mawili.
Katika
Injili ya Mathayo: 5:48 tunasoma hivi basi ninyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu
wa mbinguni alivyo mkamilifu Mungu ni wa ushirika - tasaufi ya kikristo inatuwajibisha
ulimwenguni.
Pendo la kweli lahitaji watu watatu – angalia msemo wa zamani
- wawili ni ushirika, watatu ni umati. Baba/mama/mtoto hutengeneza upendo. Huyu Mungu
tumwaminiye sisi hufahamika kwetu katika Utatu. Kidunia tunahusiana kati yetu, kimbingu
tunahusishwa na Mungu. Mimi ni mkristo kweli nikiishi katika ushirika wa upendo na
Mungu na watu wake.
Fumbo la utatu mtakatifu haliwezi kueleweka wazi. Ukuu
wake hubaki kuwa fumbo. Na leo hatutegemei kupata jibu kwa fumbo hilo. Wakristo wa
kwanza kwa akili yao walielewa ufunuo wa Baba kwa njia ya Mwanae. Yesu ameongea nasi
habari ya Baba aliyemtuma na juu ya Roho mtakatifu atakayempeleka na hii iko wazi
kwenye maandiko matakatifu.
Yesu hutuambia wazi kuwa Mungu amemkabidhi yote
naye amemkabidhi yote Roho mtakatifu. Hapa twaona muungano wa UTATU. Katika historia
ya wokovu. Mungu Baba ni mwumbaji, Mungu Mwana ni mkombozi na Mungu Roho ni Mtakatifu
hutakatifuza.
Ingawa ni nafsi tofauti Umungu ni mmoja kama ilivyokuwa kwa
Mtakatifu Agostino hatutaelewa ni kwa namna gani ila ni kwanini Mungu amejifunua kwetu.
Ukuu wa fumbo hili ni huu: sisi tumeumbwa kwa mfano na sura yake Mungu. Kwa kadiri
tunavyomuelewa Mungu ni jinsi hiyo hiyo tunavyojielewa zaidi. Wataalamu wa mambo ya
dini wanatuambia kuwa waabuduo hujitahidi kufanana na kila wanachokiabudu. Wanaoabudu
Mungu wa vita huwa watu wa vita. Wanaoabudu Mungu wa upendo huwa watu wa mapendo n.k.
Kama alivyo Mungu anayeabudiwa ndivyo walivyo wale wanaomwabudu.