2014-06-13 06:50:37

Fumbo la Utatu Mtakatifu!


Mpendwa msilikilzaji wa Neno la Mungu, leo tunaadhimisha fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni sherehe kati ya sherehe za Bwana ambayo huadhimishwa Dominika inayofuata mara baada ya Pentekoste. RealAudioMP3


Mama Kanisa ameweka sherehe hii baada ya Pentekoste kwa sababu anajua tayari fumbo zima la Utatu Mtakatifu limekwishafunuliwa kwetu. Na kwa namna hiyo Mama Kanisa apenda kutuingiza katika furaha ijayo kwetu kila siku kwa njia ya Utatu Mtakatifu. Anatushirikisha fumbo la Mungu kukaa nasi daima mpaka mwisho wa maisha ya utume wetu hapa duniani. Kwa njia ya fumbo hili upendo wa Mungu kwa wanadamu unafunuliwa hatua kwa hatua tokea Agano la kale hadi Agano Jipya.


Mpendwa msiklizaji, kwa hakika kila Dominika tunaadhimisha sikukuu ya Utatu Mtakatifu. Hata hivyo rasmi kama sherehe kati ya sherehe za Bwana, sherehe ya Utatu Mtakatifu iliwekwa katika Kalenda ya Liturujia mnamo karne XIV ili kuadhimisha na kutafakari juu ya asili ya Mungu tunayemwamini. Tunazungumza juu ya Mungu tunayemwamini, tunataka kupambanua kinaganaga tofauti na uelewa mwingine juu ya Mungu.


Mfano dhahiri ni kwamba zipo imani nyingine ambazo huamini kwamba Mungu ni muumbaji wa mbingu na nchi lakini hakushuka kuja duniani, kwa namna hiyo wanakataa asili ya utu wa Kristu. Wengine watasimama mara tu wanapofika kwa mababu. Ndiyo kusema masomo yaliyochaguliwa katika sherehe hii yanataka kuweka wazi asili ya Mungu wetu na kuondoa hisia, picha potofu na uelewa kinyume juu ya asili ya Mungu. Kwa hakika Mungu wa Kikristu si Mungu peke bali ni familia, ni UTATU.


Mmoja anaweza kukata tamaa akisikia habari ya fumbo hili kwa maana ya kuwa UMOJA usiogawanyika na wakati fulani kuonekana katika WINGI=Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mpendwa kimahesabu mantiki haitupi jibu, kumbe yatupasa kwenda katika mantiki ya Kiteolojia na Kiimani zaidi. Ndiyo kusema yatupasa kukumbuka kabisa kuwa imani si kukubali kiurahisi habari ya ukweli wa kidini bali kuukumbatia na kuuishi ukweli huo katika ugumu wake.


Mantiki hii ndiyo mantiki ya neno kuaamini kwa kiebrania. Kwa njia ya imani lazima kuweka akili zetu na maonjo yetu kwa Mwenyezi Mungu. Aidha kwa mantiki hiyo, kuwa na imani si kusadiki katika Utatu Mtakatifu tu bali kuambatana na Utatu Mtakatifu, kuishi katika Utatu na kujisalimisha na kujitumainisha katika fumbo hilo.


Katika somo Ia kwanza Mungu anajitokeza na kutangaza asili yake na hivi anarekebisha uelewa wa watu wa zamani kabla ya ufunuo huo. Watu walielewa kuwa Mungu ni mwenye nguvu, mtawala anayetisha na mwenye kuadhibu anapokosewa hasa kwa njia ya magonjwa na mikasa mbalimbali. Kumbe anatangaza asili yake kwa Musa akisema “mimi ni mwingi wa huruma, ni mwenye fadhila na si mwepesi wa hasira. Picha ya Mungu katika somo hili ni Baba, mwenye mapendo, anayeelewa shida na makosa ya watoto wake na mara moja kuwasamehe hata wanapotenda dhambi.


Katika somo la Pili toka barua ya Pili ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorinto, ambayo ni sehemu ya mwisho ya barua hiyo, Paulo anakazia maisha ya mapendo na kuheshimiana katika jumuiya. Anataja furaha, iliyo ishara ya ujio wa ufalme wa Mungu katika moyo wa mtu. Ili kuiendeleza furaha hiyo kwa ajili ya wengine anawaalika kuungana daima katika jumuiya, wakijenga amani na maelewano. Kwa furaha na mshikamano watakuwa wanaonesha sura ya Mungu katika maisha yao na kwa wengine wasioamini. Baada ya kuweka vipaji pamoja kwa ajili ya kujenga jumuiya, Mtakatifu Paulo ataweka mbele yao salaam ambayo daima huitumia kuwasalimu wanajumuiya na pengine Wakorinto walikuwa wakiitumia katika kupeana amani, yaani ile salaam inayotangaza Utatu Mtakatifu.



Kwa salaam hii Paulo ataka kuwaambia Wakorinto kuwa, ni Baba anayeanzisha safari ya kuja kwao yaani kwa ajili ya wokovu wao. Ni Baba ambaye anatunza nafasi yao huko mbinguni wa ajili ya uzima wa milele. Kisha Baba, Mt Paulo atamtaja Mwana kama yule ambaye alikamilisha nia ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Ni Mwana ambaye kwa njia ya utii na uaminifu wokovu unamfikia mwanadamu. Aidha Mtakatifu Paulo atamalizia salaam yake kwa kutangaza uwepo wa Roho Mtakatifu. Kwake yeye Roho ndiye upendo kati ya Baba na Mwana, ni yule ambaye tumepewa kwa njia ya ubatizo, na twakumbuka wote kuwa wakati tukipokea zawadi ya Roho Mtakatifu kwa njia ya ubatizo tunakuwa watoto wa Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja.


Kumbe, Mtakatifu Paulo anaposema “neema ya Bwana wetu Yesu Kristu na pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtaatifu ukae nanyi nyote, atangaza kuwa sote tunazaliwa toka Mungu mmoja. Wengine hupendekeza kama vile hii ingekuwa ndio salaam wakati wa kupeana amani, maana yaonesha umoja na mshikamano asilia wa maisha yetu ya Kikristo.


Katika Injili toka Mwinjili Yohane, tunamwona Bwana akizungumza na Nikodemo na kiini cha mazungumzo ni upendo upeo wa Mwenyezi Mungu unaojidhihirisha kwa njia ya kumtoa Mwanae wa pekee. Ni katika mazungumzo haya tunazidi kugundua asili ya Mungu, kinyume na fikra walizonazo baadhi ya watu, wakifikiri kwamba Mungu ni mpelelezi, mwenye kuadhibu na kuangamiza, kama si sasa basi anasubiri mwisho wa dunia! badala yake Mungu ni upendo usiopimika unaobubujika kila siku kwa ajili ya mwanadamu. Hili tunaligundua toka Injili ya Yohane.


Mpendwa msikilizaji, Yohane akinukuu maneno ya Bwana anasema kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminie asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maneno haya yanaonesha kuwa Mungu si tu mwenye huruma bali ni yule anayependa, kiasi kwamba anakuja kuishi kati yetu, anajimwilisha kwa ajili ya wokovu wetu! Tena huyu aliyekuja kwetu si tu alipomaliza miaka yake 33 aliondoka kwa ujumla bali anaendelea kukaa nasi katika Ekaristi Takatifu na katika sakramenti nyingine. Upendo huu upeo twaweza kujaribu kuuelewa tukirudi nyuma na kutafakari tendo la Abrahamu kutaka kumtoa sadaka mwanae wa pekee Isaka, akitufundisha uaminifu na imani kwa Mungu.


Bwana akisonga mbele katika fundisho lake wa Nikodemo anasema Mungu alipomtuma Mwana haikuwa ili Mwana auhukumu ulimwengu bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Kumbe Mwana ni kwa ajili ya kuokoa na si kuangamiza, ni kwa ajili ya kutunza na si kupatiliza mwanadamu. Bwana ametufundisha kumwita Mungu Baba “Abba” hii inawezekana kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.


Mwana ametufundisha na kutuonesha Baba ambaye hajui kulaani bali anajua kupenda tu. Bwana anasonga mbele akisema yule ambaye haamini basi anajihukumu yeye mwenyewe kwa sababu hakuliamini jina la Mwana wa pekee wa Mungu. Aya hii kama sehemu ua Injili ya Yohane inataka kujenga na kuweka wajibu wa mkristu au awaye yote mbele ya neema zinazofunuliwa kwake. Katika uhuru wake ni lazima aamue kuukumbatia upendo au kuukataa na hivi hukumu iko katika kukataa kwenyewe. Ndiyo kusema hukumu haisubiriwi siku ya mwisho bali hujifungamanisha katika kupokea au kutopokea upendo wa Mungu katika uhuru na utashi kamili wa mtu mwenyewe.


Mpendwa mwana wa Mungu, katika utangulizi nilijaribu kujenga mantiki ya Utatu Mtakatifu sasa tunaliweka fumbo katika uhalisia wa maisha ya Kanisa. Kwa kawaida ni fumbo kuu kati ya mafumbo makuu matatu, yaani fumbo la Ekaristi Takatifu na umwilisho, fumbo la neema za Mungu na Utatu Mtakatifu ambao ndio tunasherehekea leo.


Ni fumbo ambalo si rahisi kulielewa kwa undani na ukamilifu wake kwa maana ndiyo Mungu mwenyewe. Tunachotambua ni kuwa, Mungu Baba ni muumbaji, na alipokwisha kuumba mbingu na nchi alimtuma Mwanae ili aokoe mwanadamu aliyepoteza uzuri aliokabidhiwa na Mungu Baba na hivi Mungu Mwana ni Mkombozi.


Mwana alipokwisha kufundisha na kumaliza kazi yake kabla ya kupaa mbinguni alihaidi kumpeleka Roho Mtakatifu mfariji na mwalimu atakayetukumbusha yote na tena hatafanya kinyume na yale yaliyofundishwa na Bwana. Kumbe mpendwa msikilizaji Utatu Mtakatifu ni Mungu mmoja lakini nafsi tatu zisizogawanyika, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kutambua na kujaribu kuelewa tunahitaji kuwa na imani thabiti kama nilivyokwishadokeza mwanzoni.


Ninakutakieni sherehe njema, ukajazwe imani, maisha yako yote katika Utatu Mtakatifu. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.