2014-06-12 08:43:13

Papa aonya hakuna furaha ya kweli katika rushwa na ufisadi ..


Papa Francisko ameasa kwamba, ndani ya maisha ya kupenda kudhulumu wengine kwa rushwa, ufisadi, au biashara na kazi zinazokiuka utu mtu , na kumkana Mungu, maisha hayo hayana furaha ya kweli. Licha ya utajiri wa fedha na vitu wanavyoweza kujikusanyia, ndani ya mioyo yao hawana furaha. Moyoni wamejaa wasiwasi na mashaka.

Baba Mtakatifu Francisko , alionya siku ya Jumatano, wakati akitoa Katekesi kwa mahujaji juu ya vipaji vya Roho Mtakatifu. Katika katekesi hii, ambayo ilikamilisha mfululizo wa mafundisho ya Papa Francisko juu ya vipaji saba vya Roho Mtakatifu, Papa alizungumzia, kipaji cha kumcha Mungu. Alisema kumcha Mungu , haina maana ya kuwa mwoga, lakini ni kuwa wanyenyekevu na watiifu mbele ya uso wake kama vile mtoto kwa baba yake. Na kwamba sote twapaswa kufahamu kwamba , siku moja tutapaswa kutoa hesabu ya utendaji wetu Mbele yake.

Papa aliendelea kufafanua kwamba, Mungu hutupokea sisi kwa upendo mkuu. Na hivyo nasi tunatakiwa kufanya mengi mazuri kwa wengine. Lakini inahitaji kuishinda roho ya dhambi inayotuweka mbali na Mungu. Roho Mtakatifu daima yu karibu nasi kusaidia kufanya mabadiliko ya moyo na kuzungumza na Baba, Mungu wetu.

Papa alieleza na kuwataja mafisadi na wapenda rushwa kwamba , kwa nje wanaweza huonekana kuwa na furaha lakini ndani ya mioyo hao hawana amani, kwa kuwa matunda yote ya rushwa, huipotosha roho, na hukosesha ujasiri wa kwenda kwa Baba Mungu, ambaye huonekana ndani ya kuwapenda wengine.

Aidha Papa alitaja, mtu anayeishi maisha ya kudhulumu wengine na kumkana Mungu, mtu huyo hawezi kuwa na furaha, maana moyo wake uko mbali na upendo na faraja za Mungu Baba! Na aliangalisha katika matunda ya rushwa , na wale ambao wanaishi kwa mapato ya biashara ya binadamu au kwa nguvu kazi ya watumwa akisema kwamba , hata kama wanapata fedha za kutosha ndani mwao hawana furaha kamili!

Watu hawa mara nyingi hawamchi Mungu, au hujionyesha kwa nje wako karibu na Mungu lakini vitendo vy viko kinyume na mapenzi ya Mungu, hivyo wako mbali na Mungu . Papa alieleza na kutoa mfano wa wale wanao tengeneza silaha kwa lengo la kuchochea vita .. au watu ambao wanasema hawana haja ya kusikia Neno la Mungu, wanaoona wamejitosheleza wenyewe na badala yake wanazalisha vifo, wote hao hawamchi Mungu , ndiyo maana wanafanya biashara hizi za kifo. Kumcha Mungu, hutufanya kuelewa kuwa siku moja, tutatakiwa kutoa hesabu ya vitendo vyetu kwa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.