Mada zitakazojadiliwa kwenye Mkutano mkuu wa AMECEA
Kamati tendaji ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na
Kati, AMECEA chini ya Katibu mkuu wa AMECEA, Padre Ferdinand Lugonzo imetoa mada zitakazojadiliwa
wakati wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 18 wa AMECEA utakaofanyika nchini Malawi
kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 26 Julai 2014 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Uinjilishaji
kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa Imani ya Kikristo”.
Wajumbe watashirikishwa
mada inayojadili “Kazi za awali za kimissionari na hali halisi katika Ukanda wa AMECEA.
Ni mada itakayowasilishwa na wajumbe kutoka Uganda. Wajumbe kutoka Sudan katika ujumla
wao, watajadili kuhusu mazingira ya kitamaduni, kisiasa, kijamii ambamo Kanisa linaendelea
kutekeleza utume wake.
Wajumbe kutoka Tanzania wamepewa mada mbili za kujadili:
mosi ni kuhusu Uinjilishaji kama fursa inayowawezesha waamini kujikita katika wongofu
na ushuhuda wa imani ya Kikristo kwa kuweka mkazo katika maisha ya familia na jumuiya
ndogo ndogo za Kikristo. Mada ya pili itaangalia kwa namna ya pekee kabisa athari
za teknolojia ya digitali na njia za mawasiliano katika utume wa Uinjilishaji unaofanywa
na Kanisa.
Wajumbe kutoka Zambia wamepangiwa kushirikisha umuhimu wa Seminari
na nyumba za malezi katika kukuza Uinjilishaji Mpya na Malawi ambayo ni mwenyeji wa
maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 18 wa AMECEA kwa Mwaka 2014 watashirikisha kuhusu umuhimu
wa huduma za kiroho na taasisi za elimu ya juu katika kuendeleza Uinjilishaji Mpya.
Wajumbe
wa AMECEA kutoka Kenya watapembua kwa kina na mapana kuhusu Liturujia na Utamadunisho
kama njia za Uinjilishaji. Kimsingi mada saba ndizo zitakazofanyiwa kazi na wajumbe
wapatao 300 kutoka ndani na nje ya Nchi za AMECEA. Wajumbe watapata fursa pia ya kuchangia
katika majadiliano, ili kupata uelewa mkubwa zaidi.
Maaskofu wataweza kuibua
mikakati ambayo wataifanyia kazi katika mchakato wa kuimarisha shughuli za kichungaji
zinazotekelezwa na Kanisa katika nchi za AMECEA.