2014-06-11 10:25:54

Taarifa za kidemografia, kijamii na kiuchumi Tanzania


Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania tarehe 10 Juni 2014 wakati wa uzinduzi wa chapisho la tatu la taarifa za msingi za kidemografia, kijami na kiuchumi linalotokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Shukrani na Pongezi

Ndugu Wananchi;
Awali ya yote, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo. Napenda pia kuwashukuru waandaaji wa hafla hii kwa kunipa heshima kubwa ya kuzindua Chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi Linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelezo yako mazuri ya awali kuhusu Chapisho hili. Nakupongeza wewe, pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa uongozi wenu mzuri wa zoezi la Sensa. Chapisho tunalozindua leo ni matunda ya kazi nzuri mliyoifanya ya kuziongoza Idara za Takwimu za Serikali zetu mbili ambazo ndizo zilizosimamia na kuendesha zoezi lenyewe la sense ya watu na makazi.

Sensa inaendeshwa kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Takwimu (the Statistic Act) sura ya 351. Katika kipindi chote cha miaka 50 ya Muungano wetu tumefanya Sensa mara tano, mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Umuhimu wa Chapisho la Tatu

Ndugu Wananchi;

Sensa ni zoezi pana sana. Sensa ni zaidi ya kuhesabu watu. Sensa hujumuisha pia kukusanya na kufanya uchambuzi wa taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Taarifa hizo husaidia Serikali katika utungaji wa sera na kutengeneza mipango na mikakati ya maendeleo nchini. Tangu kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Idara Kuu ya Takwimu ya Taifa na Idara ya Takwimu Zanzibar ambazo ndizo zilizohusika na zoezi hili zimeendelea kutoa matokeo kulingana na kalenda ya utoaji wa matokeo ya Sensa. Matokeo ya mwanzo nilitolewa tarehe 31 Desemba, mwaka 2012 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja. Siku ile nilitangaza jumla ya idadi ya watu nchini Tanzania. Chapisho la pili lilihusu mgawanyo wa watu kwa umri na jinsi ambalo lilitolewa tarehe 25 Septemba, 2013.

Chapisho la Tatu ninalolizindua leo linatoa taarifa za msingi za kidemografia (mnyumbuliko wa idadi ya watu), kijamii na kiuchumi zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Taarifa za Chapisho la Tatu zina umuhimu wa aina yake. Zinaonesha Tanzania imepiga hatua kiasi gani katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aidha, upatikanaji wa taarifa katika kipindi hiki utaviwezesha vizazi vijavyo kuifahamu Tanzania ilivyokuwa mwaka 2012.

Muhtasari wa Matokeo ya Chapisho la Tatu

Ndugu Wananchi;

Sensa ya Mwaka 2012 imefanyika katikati ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka 5 (2011-2016). Mpango huu tunaoendelea kuutekeleza una lengo la kutufikisha kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na ile ya Zanzibar ya mwaka 2020 ambapo tunatarajia kuwa nchi yetu itakuwa imefikia uchumi wa kati. Kwa utaratibu huu wa kufanya Sensa kila baada ya miaka 10, ina maana kuwa Sensa inayofuata itafanyika mwaka 2022 ikiwa ni miaka michache kabla ya kufikia Dira ya Taifa. Hivyo, matokeo haya ni msingi wa kupima mwelekeo wetu kiuchumi na kijamii kufikia lengo letu la kuwa uchumi wa kati ifikapo 2020 kwa upande wa Zanzibar na 2025 nchi nzima.

Chapisho hili lina takwimu nyingi sana kuhusu nyanja mbalimbali za maisha ya Watanzania. Takwimu hizi zinatupa fursa ya kujua maeneo tunayofanya vizuri na yale tunayohitajika kuyaimarisha. Vilevile, zinatuonyesha yale maeneo ambayo tulidhani tunafanya vizuri lakini kumbe siyo, hivyo basi tunatakiwa kuyawekea mkakati maalum. Hali kadhalika, taarifa zinatuamsha kuona yale maeneo mapya ambayo hatukuwahi kuyafikiria lakini sasa tunapaswa kuyaangalia kwa karibu.

Kwa ujumla, kulingana na takwimu za Sensa ya 2012, idadi ya watu Tanzania iliongezeka kutoka watu milioni 34.4 mwaka 2002 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012. Hii ni sawa na kasi ya ongezeko la asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa kasi hii ya ongezeko la watu, Tanzania Bara inatarajiwa kuwa na watu milioni 63.3 mwaka 2025 ambao ndiyo mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 kwa Tanzania Bara. Aidha, Zanzibar inatarajiwa kuwa na watu milioni 1.8 ifikapo mwaka 2020 ambao ndiyo mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar. Kwa kasi hii ya ongezeko la idadi ya watu Tanzania inatarajiwa kuwa na watu milioni 125 mwaka 2050.

Ndugu Wananchi;

Ili kufikia dira zetu za maendeleo, yaani ya mwaka 2020 kwa Zanzibar na ya mwaka 2025 kwa nchi nzima ambapo tutakuwa na idadi ya watu takribanimilioni 65.1, inatupasa kujitazama tulipotoka na tulipo leo. Kwa mujibu wa Chapisho hili la Tatu, tumepiga hatua kubwa na nzuri katika maeneo mengi, na hivyo kuashiria kuwa tuko katika mstari sahihi kuelekea Tanzania tunayoitamani. Baadhi ya takwimu hizi kwa ufupi ni zifuatazo:

    Zaidi ya asilimia 90 ya watu wote Tanzania walizaliwa baada ya Muungano wa mwaka 1964. Tafsiri yake ni kwamba idadi kubwa ya Watanzania ni vijana ambao wamezaliwa, kukua na kufaidika na matunda ya Muungano. Hiki ni kiashiria kikubwa kuwa tumeweza kujenga utaifa mpya, yaani utanzania katika miaka 50 ya Muungano wetu.


    Hii ni Sensa ya tano tangu Muungano wetu mwaka 1964. Sensa ya kwanza ilikuwa mwaka 1967, ya pili mwaka 1978, ya tatu mwaka 1988, ya nne mwaka 2002 na ya tano 2012. Takwimu za Sensa za kati ya mwaka 1967 na mwaka 2012 zinaonesha kuwa idadi ya watu waTanzania ambao wanaishi mijini imeongezeka kutoka asilimia6 mwaka 1967 hadi asilimia 30 mwaka 2012. Ukuaji huu wa miji ni kiashiria muhimu kuwa safari yetu ya kuelekea uchumi wa katini ya uhakika. Hatuna budi sasa, sera na mikakati yetu kuielekeza katika kuhakikisha miji yetu inao uwezo wa kuhimili ongezeko hili la watu kwa maana ya utoaji wa huduma za kijamii na ajira.


    Katika kipindi cha miaka 50 wastani wa umri wa kuishi kwa mtoto wa Kitanzania anayezaliwa umeongezeka kutoka miaka 41 mwaka 1967 hadi kufikia miaka 61 mwaka 2012. Maana yake ni kuwa, huduma za afya zimeimarika, watu sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hata hivyo, bado hatujafikia viwango vya wenzetu wa Asia na Ulaya ambao wastani wao ni miaka 70 na kuendelea.


    Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 115 kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai mwaka 1988 hadi kufikia vifo 45 mwaka 2012. Na, mwaka 2013 tumefikia 21. Vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua kutoka 231 mwaka 1988 hadi 68 mwaka 2012 na 2013 tumefikia vifo 54 kwa 1,000. Pia, idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi imepungua kutoka vifo 578kwa kila akina mama 100,000 wanaojifungua mwaka 2004/2005 hadi 454 mwaka 2010 na kwa mujibu wa takwimu za Sensa, vifo hivi vimeendelea kupungua hadi 432 mwaka 2012. Hii ni hatua kubwa kuelekea lengo la Milenia ya Mwaka 2015 ya vifo 193.


    Asilimia ya kaya zinazopata maji safi ya kunywa imefikia asilimia 57 mwaka 2012. Vile vile, kaya zinazotumia umeme kama nishati ya kuangazia zimeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2002 hadi asilimia 21 mwaka 2012.


    Kwa upande wa sekta ya elimu, asilimia ya watu wenye umri wa miaka 10 na zaidi wanaojua kusoma na kuandika kwa Tanzania Bara imeongezeka kutoka asilimia 31 mwaka 1967 hadi kufikia asilimia 78 mwaka 2012. Kwa Zanzibar kiwango hiki kimeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 1967 hadi asilimia 86mwaka 2012.


    Takwimu zinazoonesha kwamba umaskini wa kipato umepungua kutoka asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012.


    Takwimu zinaonesha kwamba makazi ya wananchi wote wa Tanzania yaliyojengwa kwa vifaa vya kisasa (zege, mawe, saruji na vyuma) yameongezeka. Familia zinazoishi kwenye nyumba za bati zimeongezeka kutoka asilimia 46mwaka 2002 hadi asilimia 65 mwaka 2012.


    Vilevile, umiliki wa simu za kiganjani umeongezeka sana. Mwaka 2012 wastani ulikuwa ni asilimia 64ikilinganishwa na asilimia 10 mwaka 2005. Kuongezeka kwa simu ni kiashiria cha kuongezeka kwa biashara, idadi ya watu wanaotumia huduma za kifedha kwa njia ya simu na urahisi wa mawasiliano ambao unawezesha usambazaji wa taarifa za kijamii na kibiashara katika maeneo mengi hivi sasa.


Mazingatio Yatokanayo na Chapisho la Tatu la Sensa

Ndugu Wananchi;

Ufupi au urefu wa safari unaweza kuujua tu iwapo unafahamu unapotoka, ulipo na unapokwenda. Taarifa ambazo zimewasilishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa tumepata mafanikio ya kuridhisha katika maeneo mengi, na kuwa tumekuwa tunasonga mbele mwaka hadi mwaka na siyo kurudi nyuma. Kwa hiyo matokeo haya yanapaswa kuwaongoza Viongozi na Watendaji wa ngazi zote katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kujua maeneo ambayo kasi ya utekelezaji wa programu za maendeleo kwa wananchi ilikuwa ndogo, na hivyo kustahili kupewa msukumo mpya katika utekelezaji wake.

Ndugu Wananchi;

Nimefarijika kusikia kuwa taarifa za Sensa zinaonesha hatua kubwa tuliyopiga katika kuleta usawa wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake. Ingawa viashiria vingi bado vinaonekana bora zaidi kwa wanaume kuliko wanawake, lakini pengo kati yao limepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma. Kwa mfano, asilimia ya wanaume wenye umri wa miaka 10 na zaidi wanaojua kusoma na kuandika ilikuwa asilimia 45 kwa Tanzania Bara na asilimia 55 kwa Zanzibar mwaka 1967. Kwa upande wa wanawake ilikuwa asilimia 19 na asilimia 23 kwa Tanzania Bara na Zanzibar mwaka 1967. Taarifa za Sensa ya Mwaka 2012 zinaonesha kuwa pengo hili limepungua sana. Wanaume wenye umri wa miaka 10 na zaidi wanaojua kusoma na kuandika kwa mwaka 2012 ni asilimia 82 ya wanaume wote kwa Bara ukilinganisha na asilimia 75 kwa wanawake. Kwa upande wa Zanzibar, idadi ya wanaume wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia 89 ya wanaume wote kulinganisha na asilimia 83 ya wanawake.
Hatuwezi kupata maendeleo makubwa na endelevu bila kuhakikisha usawa wa kijinsia. Wanawake ni asilimia 51 ya Watanzania wote, hivyo, hatuna namna yoyote tunayoweza kulipuuza kundi hili kubwa, ambalo ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote katika shughuli za maendeleo. Ndiyo maana, tumeelekeza juhudi kubwa kurekebisha kasoro hii ya kihistoria na kimfumo kwa kuwapa wanawake fursa ili nao washiriki sawia katika shughuli za maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na hata taifa. Ni vyema ikaeleweka kuwa hatuwapendelei wanawake bali tunawapatia kile wanachostahili kupata kama raia na kama wanadamu. Stahili ambazo wamekuwa wakizikosa kwa miaka mingi.

Serikali itaendelea kuimarisha juhudi za utekelezaji wa Sera ambazo zinalenga kuhakikisha kuwa pengo hili linazibika ili Watanzania wote wafaidike na rasilimali za Taifa bila ya kujali jinsia zao.

Maelekezo kwa Tume ya Taifa ya Takwimu
Ndugu Wananchi;

Nimesema hapo awali kuwa lengo kubwa la kufanya Sensa ni kutoa takwimu ambazo zitachangia katika jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania. Taarifa za sensa ambazo zitasaidia kuboresha sera za nchi kwa mambo mbalimbali, kupanga na kutathmini programu za maendeleo na uimarishaji wa utoaji wa huduma za jamii. Lengo hili haliwezi kufikiwa ikiwa taarifa za sensa na nyinginezo kwa ujumla wake hazitawafikia watumiaji wote wanaozihitaji. Ofisi za Takwimu zina jukumu la kutoa takwimu katika mfumo mzuri na lugha rahisi na kuzisambaza na kuhamasisha matumizi yake.

Pamoja na usambazaji wa taarifa za sensa kwa vitabu na machapisho, tumieni tovuti na njia nyingine za kisasa kusambaza taarifa zenu. Ninafarijika kusikia kwamba tayari mmeanza juhudi hizi, kwani uzinduzi wa Chapisho hili la tatu utaenda sambamba na uzinduzi wa usambazaji wa taarifa kwa njia ya mtandao.

Ofisi za Takwimu zimetimiza wajibu wake wa kutoa takwimu na sasa ni jukumu la Wizara, Idara,Taasisi za Serikali na watumiaji wengine wote kuzifanyia kazi. Natoa agizo kwa viongozi ngazi zote za utawala kutafsiri matokeo haya kwa kuoanisha na utekelezaji wa sera na programu za maendeleo ya kisekta katika maeneo yao. Matokeo haya ya Sensa sasa ndiyo rejea yetu ya takwimu katika mipango yetu ya utekelezaji.

Kile kisingizio cha kukosekana kwa takwimu mpya sasa kimefikia ukomo. Takwimu ni kitendea kazi, sasa mnazo na mkazifanyie kazi, siyo kuendeleza semina za kujadili matatizo na mapungufu. Takwimu zimetuonyesha mafanikio tuliyoyapata na mapungufu yaliyopo ambayo mkayatatue na siyo kuyajadili.

Wito kwa Wananchi na Wadau
Ndugu Wananchi;

Napenda pia kutoa wito kwa wananchi na wadau wa maendeleo hasa asasi za kiraia kusoma taarifa hizi na kuzitumia vizuri. Kumekuwepo na upotoshaji mkubwa sana wenye kubeza mafanikio yaliyopatikana nchini kutokana na jitihada za Serikali na wananchi kwenye kuleta maendeleo. Taarifa hii inaweka wazi ukweli ulivyo. Zitumieni. Kama upotoshaji ulikuwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa rejea ya takwimu sahihi, takwimu ndizo hizo kwa kila mmoja wetu kuziona na kuzitumia. Asiyefanya hivyo ana lake jambo.

Hitimisho

Ndugu Viongozi Wenzangu;
Ndugu Wananchi;

Niruhusuni nirudie tena kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo waliotusaidia kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi. Kwa namna ya pekee nawashukuru Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Taasisi za Umoja wa Mataifa ikiwemo UNFPA, UNDP na UNICEF. Nawashukuru tena Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda na Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Idd kwa uongozi wenu mzuri uliowezesha zoezi zima la sensa kufanikiwa. Pia, nawapongeza viongozi na watendaji wa Idara zetu mbili za Takwimu kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Umakini na umahiri wao ndiyo uliotufikisha hapa.

Nawashukuru na kuwapongeza viongozi wote wa Serikali wa ngazi zote za utawala ambao walishiriki kwa ukamilifu katika maandalizi na hatimaye utekelezaji wa Sensa ya Mwaka 2012. Nitoe pia shukrani kwa viongozi wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa ushiriki wenu hasa kwenye hatua ya uhamasishaji wa ushiriki wa umma. Nawashukuru wadau wetu wa maendeleo kwa michango yao muhimu ambayo imesaidia kufanikisha sensa hii.

Shukrani za kipekee ziwaendee Wananchi wote ambao walijitokeza kuhesabiwa na kujibu maswali ya sensa kwa ufahamu mkubwa. Kukubali kwao kushiriki ndiko chanzo kilichowezesha kupatikana taarifa tunazozindua leo na nyingine zitakazofuata. Ni dhahiri kuwa Serikali yetu imetimiza kwa ufanisi jukumu la kufanya Sensa ya Watu na Makazi nchini. Lengo limetimia la kujua hali halisi ya rasilimali watu iliyopo Nchini kama zilivyofanya Awamu zote zilizotangulia.
Ndugu Wananchi;

Baada ya kusema maneno haya ya utangulizi, sasa, kwa heshima na taadhima kubwa, napenda kutamka kwamba Chapisho la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Pamoja na Matumizi ya Tovuti katika kupata taarifa mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi limezinduliwa rasmi.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza!








All the contents on this site are copyrighted ©.