2014-06-11 07:27:00

Nyanyaso za kijinsia na ubakaji ni mambo ambayo hayakubariki tena!


Bwana Nigel Marcus Baker, Balozi wa Uingereza mjini Vatican anasema kwamba, unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji ni kati ya matendo ya kikatili wanayofanyiwa wanawake nyakati hizi hasa katika maeneo ambamo mtutu wa bunduki unashika hatamu. Ubakaji katika maeneo ya vita ni vitendo ambayo vinaendelea kushamiri kiasi cha kunyanyasa utu na heshima ya wasichana na wanawake.

Wanajeshi wanaojihusisha na vitendo hivi wanataka kuwajengea watu hofu, kujitwalia madaraka na kudhibiti maeneo wanayojinyakulia kinyume cha sheria. Ikumbukwe kwamba, hata vita inapotimua vumbi, kuna sheria za kimataifa ambazo zinapaswa kufuatwa. Kwa bahati mbaya wahusika wengi wa vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia bado hawajafikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Watu hawana budi kujikita katika mchakato wa majadiliano ili kumaliza migogoro na kinzani za kijamii kwa njia ya amani na kwa nafasi hii, vitendo vya unyanyasaji na ubakaji vinaweza kutoweka ndani ya jamii. Kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 13 Juni 2014 kunafanyika mkutano wa kimataifa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ubakaji mjini London, Uingereza. Mkutano huu unalenga kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyofanywa wakati wa vita.

Wadau mbali mbali wanatakiwa kujifunga kibwebwe ili mkutano huu uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani kulinda na kudumisha utu na heshima ya wanawake, kwani madhara ya vitendo kama hivi yanadumu katika maisha ya wahusika kwa kipindi kirefu; hii ni aibu ya wahusika na familia zao. Mkutano huu unapania pamoja na mambo mengine kuweka kumbu kumbu za vitendo vya unyanyasaji kijinsi, ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kuweka sahihi itifaki itakayopiga rufuku vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia wakati wa vita.

Ni matumaini ya Balozi Baker kwamba, serikali mbali mbali zitaunga mkono juhudi hizi, kwa kuhakikisha kwamba, sheria za nchi zinakidhi viwango vya kimataifa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ubakaji na kwamba, wahusika wanafikishwa mbele ya sheria. Wanajeshi nao wanapaswa kubadilisha mtindo wa maisha na kuachana kabisa na vitendo vya ubakaji, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia.

Viongozi mbali mbali wa kidini wanashirikisha pia mchango wao katika mapambano dhidi ya vitendo hivi vichafu katika jamii. Mtandao wa mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki kimatifa umekuwa mstari wa mbele kuwasaidia na kuwajengea uwezo wanawake wanaokumbana na majanga katika maisha hasa wakati wa vita! Mkutano huu unahudhuriwa na wawakilishi zaidi ya 100 kutoka katika nchi mbali mbali na kuna wataalam 900, wote hawa wanataka kuhakikisha kwamba, nyanyasao za kijinsi zinapata ufumbuzi wa kudumu!







All the contents on this site are copyrighted ©.