2014-06-10 06:51:32

Kongamano la Utoto Mtakatifu nchini Tanzania


Kanisa Katoliki linaendelea kuwekeza katika malezi na makuzi ya watoto kwa kuwajengea maisha ya sala, umoja, udugu na mshikamano kwa kutambua kwamba, watoto ni taifa la kesho, kumbe, changamoto kubwa iliyoko mbele ya Familia ya Mungu ni kuhakikisha kwamba, kwa pamoja inashiriki katika kuwalea watoto ili wakue katika imani ya Kikristo, maadili na utu wema! RealAudioMP3

Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 – 16 Juni 2014 yatafanya Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu, Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi na kuongozwa na kauli mbiu “Nimtume nani? Niko hapa nitume mimi”. Rai ya Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari nchini Tanzania inasema kwamba, watoto waliolelewa katika imani ya Kikatoliki ni nguzo za Kanisa Katoliki na Jamii nzima.

Katika kongamano hili la kitaifa litakalowajumuisha watoto kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania litajadili pamoja na mambo mengine kuhusu: Mtoto na imani; Watoto na athari za utandawazi; Watoto na maisha ya Sakramenti hasa Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Haki za watoto na wajibu wao kwa wazazi na walezi; wajibu wa wazazi katika malezi ya watoto; Watoto na maisha ya watakatifu; Watoto na utume wa umissionari; Watoto na miito mitakatifu.

Watoto pia wataangalia wajibu wao kama sehemu ya matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa imani uliotishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kuadhimishwa kwa kishindo na Papa Francisko. Askofu Castor Msemwa wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi ndiye mwenyeji wa kongamano la kitaifa la Utoto Mtakatifu nchini Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.