2014-06-09 07:23:50

Usidandie karama utateseka!


Kadiri ya Kalenda yetu ya Kiliturujia, tukifuata mapokeo ya tangu zamani za wazee wetu, siku ya hamsini baada ya ufufuko wa Bwana, Kanisa linaadhimisha sherehe ya Pentekoste. RealAudioMP3

Katika adhimisho hili, ndipo haswa tunapokumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na kuanza rasmi kwa utume-hadhara wa Mitume wa Yesu. Kristo Bwana kama daima katika mafundisho yake alivyowaahidia Roho Mtakatifu, atakayefanya kazi ya kuwafundisha na kuwakumbusha yote aliyapata kuwafundisha, Roho huyo anawashukia Mitume (walipokuwa wakisali ndani ya chumba chsa juu), na mara wanaanza utume hadhara unaoambatana na ishara za kunena kwa lugha. Ni kwa roho huyo, mitume walipokea karama kwa ajili ya utume.

Sisi nasi, tunampokea Roho Mtakatifu kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Kipaimara. Tendo lile tunaliita ni Pentekoste binafsi ya kila mbatizwa. Na kutoka hapo, tunaimarishwa nasi ili tuwe askari shujaa wa Kristo Yesu, kwa ajili ya kutangaza, kulinda na kuuishi ukweli wa injili kama alivyotufundisha Yesu mwenyewe. Katika kufanya hivyo, tunasaidiwa na Roho wa Mungu yule yule mwenye kututia nguvu. Roho huyo anatujaza mapaji ya kutuwezeshsa kuushi vema Ukristo wetu. Katekisimu yetu inatufundisha juu ya mapaji saba ya Roho Mtakatifu, ambayo ni hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji wa Mungu.
Haya mapaji ni ZAWADI ya Mungu kwa kila mmoja wetu. Mtume Paulo anatualika sasa kutumia mapajia haya kwa ajili ya kuwafaidia wengine, kwani mapaji haya ni kwa ajili ya HUDUMA katika maisha yetu ya kila siku. Kila mmoja amejaaliwa tofauti kadiri Mungu anavyotaka, na kadiri mwanadamu mwenyewe anavyopokea zawadi hii. Lakini Roho Mgawaji wa mapaji ni YULEYULE.

Mtume Paulo anasema “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” 1Kor. 12:4-11.

Mwaliko tunaupeleka katika Kanisa la nyumbani (yaani katika familia), kwa vile “... pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom. 5:5), basi katika familia tusaidiane kutambua vema na kufuata karama zetu. Hili kwanza kabisa ni jukumu la wazazi kwa watoto wao, na wote wenye dhamana ya malezi. Katika Roho ya sala na usikivu kwa Roho Mtakatifu, wazazi someni karama za watoto wenu na wasaidieni kukua huku wakitii karama hizo katika roho ya uadilifu. Ni kwa njia hiyo tu familia inashiriki katika kuwaunda mitume wa Kristo kwa ajili ya ulimwengu wa leo.
Mtume Paulo katika andiko tulilolisikia, anaonesha wazi kwamba, karama tulizonazo ni kwa ajili ya huduma kwa wengine. Endapo mtoto hatasaidiwa kutambua na kuikuza karama yake, baadaye atafanya kazi isiyo yake na matokeo yake ni kuharibu usitawi wa watu. Ni bahati mbaya sana nyakati zetu hizi, kwa sababu ya upofu-baridi katika kusaidia watoto wetu kukuza karama zao, watoto wetu/vijana wetu wanapoteza mwelekeo wa maisha mapema sana. Kwa sababu ya kutojua nini amejaaliwa kufanya katika maisha, mwishoni wazazi wanampeleka afanye kazi yoyote ile, alimradi atalipwa.

Wengi wanaitwa waalimu huko mashuleni, lakini sio karama zao, unaona wanavyoteswa darasani. Wengi wanaitwa waganga/wauguzi lakini sio karama zao, wamedandia karama za wengine, utawaona tu wanavyokuwa wazembe katika kuhudumia wagonjwa na hata kuua watu. Kuna wanaohudumu katika mabenki, kumbe wana alergy na hesabu, utaona wanavyopindisha mahesabu kila siku. Kwa bahati mbaya kubwa, unaweza kuona pia wapo watakaoitwa makuhani au watawa, kumbe sio wito wao, wamedandia wito wa wengine, utaona jinsi wanavyoleta vituko kila siku, wanavyokosa furaha na wasivyopenda utume.

Ukiona mtu ni mhovyohovyo katika kazi yake ya kuwahudumia watu, ukichunguza vizuri, utagundua kuwa sio wito wake. Mfano ukamwona muuguzi, ambaye anapaswa pia kuwa mvumilivu na mfariji mwenye huruma, anakuwa mkali kwa wagonjwa, anawahudumia akiwa amekunja pua kama ananusa sumu, lugha korofi kila wakati, jua kuwa huyo, huenda alikuwa na wito wa askari wa wanyama-pori, ila hakujua karama yake, sasa ameparamia uuguzi, matokeo yake, atawatendea wagonjwa kama wanyama-pori vile.

Hali hii inatokana na kutokutambua na kutokuiitikia karama halisi uliyopewa na Mungu. Kanisa la nyumbani ndiyo kitalu cha kusitawisha mitume na wahudumu mbalimbali. Wazazi, leeni watoto wenu. Vijana, ombeni hekima ya Mungu iwasaidie kujua karama zenu halisi ili muwe watumishi wema kwa Kanisa na Taifa.

Lakini pia, tutoe angalisho la kichungaji: Leo hii, wengi wamegeuza karama kuwa ni biashara. Kuna kasi kubwa ya kutafuta pesa kwa njia ya karama za huduma tulizopewa. Na ndiyo maana, tunakuta watu wengi wanalazimisha baadhi ya karama ili tu wachume pesa. Mtume Paulo anataja karama za kutenda miujiza na uponyaji. Wajanja wengi, kwa kujua kuwa wanadamu wa leo tumetembelewa na magonjwa mengi, na tumegubikwa na hamu ya kutafuta mafanikio ya haraka, ndipo unaona waponyaji-koko wanazuka na watenda miujiza-viigizo.

Nguvu hiyo wanapata wapi?? Wenyewe mwajua!! Roho hiyo ya kupenda miujiza ndiyo mlango mkubwa unaotupeleka katika kumtafuta na kumsujudu shetani. Wapenda miujiza na walazimisha-karama mwisho wao huwa ni aibu, kufilisika sana na kupoteza mwelekeo. Usichanganye Mungu na shetani, UTAUMIA!!

Tambua karama yako, ikuze na uitumie kwa nguvu ya Mungu. Na papo hapo, heshimu karama za wengine. Kwa sababu nao pia wamepewa na roho yuleyule. Usidharau kipaji cha mtu. Na wala usifikiri hata siku mmoja kwamba wewe umejaliwa zaidi na yule amejaliwa kidogo, hapana. Mungu huwa anatoa karama ya kutosha kwa kila mmoja wetu, kwa ajili ya utume, uliokusudiwa. Basi, na tumwombe Mungu, ili kwa nguvu ya Roho wake tuwe mitume wema.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.