2014-06-09 08:02:40

Nguvu ya Sala nchini Nigeria!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limeamua kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Nigeria kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Julai hadi Desemba 2014 kutokana na kukithiri kwa mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram. Kila mwezi, Kanisa nchini Nigeria litakuwa na nia maalum: kwa mwezi Julai, waamini watasali kwa ajili ya kuachiliwa huru kwa wasichana wa shule waliotekwa nchini Nigeria.

Mwezi Agosti, Kanisa litawakumbuka waathirika wote wa vitendo vya kigaidi nchini Nigeria. Mwezi Septemba, waamini watasali kwa ajili ya kuwaombea askari wa vyombo vya ulinzi na usalama waliojisadaka kwa ajili kutekeleza dhamana yao ya ulinzi na usalama kwa wananchi wa Nigeria na mali zao, kati yao kuna baadhi wamepoteza maisha na wengine kupata vilema!

Mwezi Oktoba, Kanisa kwa namna ya pekee litaombea umoja wa kitaifa, amani na utawala bora; mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Nia za Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwa Mwezi Novemba ni kuombea mapambano dhidi ya rushwa ili kudumisha misingi ya haki na amani.

Kwa mwezi Desemba, Kanisa Katoliki nchini Nigeria litaelekeza nia na maombi yao kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza tunu msingi za maisha ya kifamilia pamoja na kusimama kidete kutetea Injili ya Uhai. Kadiri ya maelekezo yaliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, waamini wanahimizwa kusali kama mtu binafsi, familia, kigango, Parokia na Jimbo. Sala hii inaweza kuwa ni tafakari ya Rozari Takatifu, muhtasari wa kazi ya Ukombozi, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu mwishoni mwa kila mwezi.

Katika ngazi ya kitaifa kutakuwa na hija ya kitaifa itakayofanyika tarehe 13 - 14 Novemba 2014 katika Kituo cha Kiekumene, Jimbo kuu la Abuja, Nigeria. Baada ya matumizi ya mtutu wa bunduki kushindwa kuwapatia wananchi wa Nigeria amani na utulivu, sasa Maaskofu wanataka kumlilia Mfalme wa Amani ili aweze kusaidia juhudi za upatikanaji wa amani na utulivu nchini Nigeria, kwani watu wamechoshwa na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, wamechoshwa na mashambulizi yanayowanyima amani na utulivu; wamechoshwa na vitisho vinavyowajengea wananchi hofu na mashaka katika maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.