Marais Shimon Peres na Abbas Mahmoud waungana na Papa kuomba amani
Jumapili 08 June 2014, majira ya Alasiri, ulikuwa ni wakati nadra wa kihistoria ,
ndani ya Bustani za Vatican, ambako kulifanyika mkutano wa sala kwa ajili ya kuombea
amani. Rais Shimon Peres wa Israel na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, waliketi
pamoja karibu karibu, wakiitikia mwaliko wa Papa Francisko, alioutoa wakati akifanya
hija katika Nchi Takatifu mwezi jana. Sala hii ilifanyika mbele ya Patriaki wa Constantinople,
Bartholomayo I na Msimamizi wa Maeneo Matakatifu katika Nchi Takatifu Padre Pizzaballa,
wakiwepo pia wageni wengine waalikwa. Sala zilitolewa katika lugha mbalimbali, lakini
zote zikilenga katika nia hiyo ya kuomba amani kwa Mashariki ya Kati na dunia kwa
ujumla . Baadaye Hotuba ya Papa Francisko, ilifuatiwa na hotuba za Marais hao wawili
na mkutano binafsi.
Taarifa zinasema, wakati huo , ulikuwa ni wakati wa kusisimua
kwa viongozi hao watatu, ambao walikumbatiana kwa moyo wa udugu na upendo , wakimtolea
Mungu muumbaji shukurani , kuomba msamaha, na kuombea amani. Amani kati ya watu,
Wayahudi, Wakristo na Waislamu na amani katika Nchi Takatifu, ni msisitizo ulitolewa
na Papa na Marais hao wawili katika hotuba zao.
Papa Francisko , alionyesha
tumaini kubwa kwamba, kukutana ana kwa ana kwa Marais hao, itakuwa ni mwanzo wa njia
ya kutafuta mikakati mipya ya kuwaunganisha na kuondokana na mgawanyiko wa siku nyingi.
Papa akiongoza maombi ya watu wengi wenye mapenzi mema waliokuwa wamefikla katika
bustani hizo wa dini, tamaduni na mataifa mbalimbali, aliomba, ili kwamba, atoe
jibu kwa hamu ya wakereketwa wote, wanao tamani amani na kuwa na ndoto ya dunia
ambayo wanaume na wanawake wanaweza kuishi kama ndugu na si kama wapinzani au maadui.
Papa aliwakumbusha kwamba, dunia ni urithi tulioupokea kutoka kwa mababu
zetu. Na pia ni kweli tu kwamba, ni dhamana tuliyokabidhiwa kwa ajili ya watoto wetu:
wana ambao wamechoshwa na kudhoofishwa na migogoro na sasa wana hamu ya kuona mapambazuko
mapya ya amani. Wana wanaotutaka tuvunje kuta za uadui na kuchukua njia ya mazungumzo
na amani kwa upendo na ushindi wa urafiki .
Papa Francisko aliendelea katika
hotuba yake kuwakumbuka pia wale wote waliopoteza maisha yao katika vurugu na vita,
ili kwamba sadaka ya maisha yao isipotee bure. Na hivyo aliwaomba wageni wake, Peres
na Abbas, kuwa na ujasiri wa amani, wa kudumu katika mazungumzo kwa gharama zote,
na kuwa na subira katika michakato thabiti lakini yenye kufanyika kwa amani, kuheshimiana
na mshikamano.
Papa aliasa kutengeneza amani kunahitaji ujasiri, kuliko
vita. Kunahitajika ujasiri wa kusema ndiyo katika , kuketi kwenye mikutano na si
mapambano; ndiyo katika mazungumzo na si vurugu; ndiyo katika kukataa mazungumzo yenye
kujenga uadui na machukizo. Ni kusema ndiyo katika kuheshimiana , na hapana katika
kuwa wanafiki. Kwa haya yote, kunahitajika ujasiri, ujasiri mkubwa. Papa alisisitiza.
Ili kuweza kuifikia amani hiyo , kunahitajika msaada wa Mungu . Papa alieleza
na kwa kurejea historia ambayo inatufundisha kwamba nguvu ya vikosi vya binadamu peke
yake haitoshi kufanikisha amani. Hivyo kuna haja ya kuinua macho yetu yote mbinguni
na kwa utambuzi kwamba, sisi sote tu watoto wa Baba mmoja. Papa alifunga hotuba
na sala ya kuomba msaada wa maombezi ya Mama Bikira Maria , na neno 'amani, shalom,
salam',liwe neno la siku zote katika maisha yetu.