2014-06-08 09:17:06

Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Juni 2014 amewapongeza vijana wanaofanya hija ya 36 ya maisha ya kiroho kutoka Macerata kuelekea Loreto katika mkesha wa Siku kuu ya Pentekoste na anataka kuwahakikishia uwepo wake wa kiroho katika tukio hili muhimu katika maisha yao ya kiroho. Anawashukuru na kuwapongeza kwa kuendelea kuombea amani huko Mashariki ya Kati, ili dunia iweze kusikia kwa mara nyingine tena ule wimbo wa Malaika "Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema".

Baba Mtakatifu ametuma ujumbe huu kwa njia ya simu na kuzungumza na vijana hawa moja kwa moja kutoka mjini Vatican. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni "Mwenyezi Mungu mwingi wa miujiza", jambo ambalo ni kweli, kumbe vijana hawana budi kushangaa, kuomba na kumuuliza Mwenyezi Mungu ili kukuza na kudumisha zawadi ya imani ambayo wanakirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Hii ni zawadi ambayo wanapaswa kuiboresha kwa uvumilivu, mafanikio na wakati mwinginie kwa shida na magumu, lakini hakuna sababu ya kuogopa kwani Mwenyezi Mungu atawabariki na kuwakirimia kadiri ya mahitaji yao! Kamwe vijana wasiwaogope wale wanaotaka kuwapokonya ndoto hii njema na badala yake, watoe kipaumbele cha kwanza kwa mwanga wa matumaini, wakiwa na mwelekeo chanya wa maisha unaojikita katika furaha wanayowashirikisha wengine.

Matumaini kamwe hayawezi kudanganya na kwa Mungu hakuna kinachoweza kupotea, lakini bila Mungu yote ni ubatili mtupu! Huu ni mwaliko kwa vijana kumfungulia Mungu malango ya mioyo yao, ili macho yao yaweze kuona tena njia na matendo yake makuu!







All the contents on this site are copyrighted ©.