2014-06-08 11:58:47

Roho Mtakatifu anafundisha, anakumbusha, anasali na kufanya unabii!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste, tarehe 8 Juni 2014 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa mahubiri yake anasema kwamba, Yesu aliwaahidia Mitume wake zawadi kutoka kwa Baba, yaani Roho Mtakatifu na ahadi hii inatekelezwa wakati wa Siku kuu ya Pentekoste.

Hili ni tukio endelevu linaojionesha katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Roho Mtakatifu analihuisha Kanisa, anawafundisha, anawakumbusha na kuwasaidia waamini kuzungumza.

Papa Francisko anasema, Roho Mtakatifu ni mwalimu wa maisha yandani anayewaonesha waamini dira na njia ya maisha kama alivyofanya wakati wa Kanisa la mwanzo. Roho Mtakatifu ni njia kama alivyo Yesu mwenyewe, kwani anawasaidia waamini kumfuasa Kristo na kutembea katika nyayo zake. Roho Mtakatifu ni mwalimu wa maisha, ujuzi na maarifa katika uwepo na utume wa maisha ya Kikristo.

Roho Mtakatifu anawakumbusha waamini yale ambayo Yesu amewafundisha mitume wake, ni kumbukumbu hai ya Kanisa anayewakumbusha waamini uwepo endelevu wa Kristo katika maisha na utume wa Kanisa. Ni Roho wa ukweli na upendo anayedai jibu makini kutoka kwa waamini kwa njia ya maneno ya Yesu yaliyomwilishwa katika ushuhuda wa maisha pamoja na kukumbushwa kuiishi ile amri kuu ya mapendo kwa Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amewataka waamini kuzingatia umuhimu wa historia ya Ukristo kwa kuisoma na kuimwilisha kama sehemu ya histoaria ya ukombozi na kwamba, Roho Mtakatifu anawasaidia kuyaangalia yote haya katika mwanga wa mafundisho ya Yesu na hivyo kukuza hekima moyoni ambayo kweli ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Roho Mtakatifu anawajalia waamini kumbukumbu ya kuweza kuzungumza na Mungu pamoja na wengine kwa njia ya sala kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wateule wa Mung. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kushiriki katika majadiliano ya kidugu ili kujenga na kuimarisha urafiki, amani na utulivu kwa kutambua mateso na matumaini; wasi wasi na furaha kwa wengine.

Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuwa kweli ni Manabii wanyenyekevu wa Neno la Mungu, ili kukemea kinzani na ukosefu wa haki, ili kuponya na kujenga kwa kutumia upendo, ili kweli waamini waweze kuwa ni vyombo vya Mungu anayependa, anayehudumia na kugawa zawadi ya uhai.

Kwa ufupi Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu anawafundisha waamini njia ya maisha, anawakumbusha na kuwafundisha Maneno ya Yesu; anawasaidia kusali na kumwita Mwenyezi Mungu, Abba, yaani Baba; anawafundisha kujadiliana na wengine na kuonesha unabii.

Siku kuu ya Pentekoste ni siku ya Ubatizo wa Kanisa linalotumwa kuwatangazia watu wote Habari Njema ya Wokovu. Mitume kwa kupokea nguvu ya Roho Mtakatifu wanaanza kutekeleza utume wao wa Kuinjilishaji kwani bila Kristo hakuna Uinjilishaji, ndiyo maana Kanisa linamwita na kumwomba Roho Mtakatifu!







All the contents on this site are copyrighted ©.