Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawapongeza askari wote wa vyombo
vya ulinzi na usalama wanaotoa huduma mjini Vatican kwa kazi kubwa na nzuri wanaoitekeleza
katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza kwa weledi,
majitoleo, dhamana na uwajibikaji wao katika masuala ya ulinzi na usalama mjini Vatican
na kwa ajili ya wote wanaofika Roma kufanya hija kwenye makaburi ya watakatifu Petro
na Paulo bila kuwasahau wanaofika kumsikiliza Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Kardinali
Parolin ameyasema hayo Jumamosi, tarehe 7 Juni 2014 wakati wa maadhimisho ya Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama wanaotekeleza
majukumu yao mjini Vatican. Hii ni huduma inayotekelezwa kwa hali ya unyenyekevu na
majitoleo makuu; katika utulivu na huduma kwa Jamii. Vatican ni mji ambao una utajiri
mkubwa wa sanaa, lakini umesheheni idadi kubwa ya mahujaji wanaofika kusali na kushuhudia
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa ni kivutio kikuu cha watalii kutoka sehemu
mbali mbali za dunia. Vatican ni makao makuu ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na
la mitume!
Huduma inayotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama inawawezesha
watu kuonja amani na utulivu mioyoni mwao, kiasi cha kuendelea kumwimbia Mwenyezi
Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya zawadi ya imani kwa Yesu Kristo Mnazareti.
Kanisa linaendelea kumshukuru Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu,
changamoto kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo
na Kanisa lake pamoja na kumtegemea Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa katika maisha
na utume wake.
Kardinali Pietro Parolin anawataka waamini kujenga moyo wa ibada,
heshima na kuaminiana kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na
utume wa Kanisa, wakiongozwa na upendo kwa Mungu na jirani. Kila mwamini ajitahidi
kuwa ni shahidi na mtangazaji wa Yesu Kristo Mfufuka mintarafu huduma anayoitoa mbele
ya jamii.