Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Juni 2014 amekutana na kuzungumza na Rais
Enrique Pèna Nieto wa Mexico na baadaye pamoja na ujumbe wake wamekutana na kuzungumza
na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu
mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa
mjini Vatican.
Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais wa Mexico,
kwa pamoja wamegusia hali ya maisha nchini Mexico pamoja na kuangalia mabadiliko mbali
mbali yaliyofanywa nchini humo hususan katika Katiba ya Nchi inayojadili kwa namna
ya pekee uhuru wa kidini. Viongozi hawa wawili wamezungumzia pia masuala mbali mbali
kama vile uhamiaji, mapambano dhidi ya baa la umaskini, ukosefu wa fursa za ajira
pamoja na mikakati ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Mwishoni,
Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamebadilishana mawazo kuhusu masuala ya kitaifa na
kimataifa!