Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda limeishukuru Serikali ya Uganda kwa kuhakikisha
ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashahidi wa Uganda iliyofanyika
hivi karibuni pamoja na kuwashukuru viongozi mbali mbali wa Serikali walioshiriki
katika maadhimisho haya kielelezo cha umoja na mshikamano katika mambo msingi.
Hayo
yamebainishwa na Padre Philip Odii, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda
wakati wa mahojiano maalum na Gazeti la AMECEA linalochapisha habari zake kwenye mtandao.
Serikali ilihakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama vinatekeleza wajibu wake
barabara ili kuwawezesha waamini kutoka ndani na nje ya Uganda kuadhimisha kumbu kumbu
ya Mashahidi wa Uganda kwa amani na utulivu, kielelezo makini cha utekelezaji wa uhuru
wa kuabudu, dhidi ya vitisho vya mashambulizi ya kigaidi ambavyo vimeendelea kuwajengea
watu hofu kubwa katika siku za hivi karibuni.
Viongozi mbali mbali wa kidini
na serikali wanaendelea kuwaonya wananchi wa Uganda kuwa makini dhidi ya watu wanaoweza
kujipenyeza nchini humo na hivyo kusababisha vitendo vya kigaidi.
Ibada ya
Misa Takatifu iliyongozwa na Askofu Giuseppe Filippi kutoka Jimbo Katoliki la Kotido,
Uganda. Katika mahubiri yake, amewaonya waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutomezwa
na malimwengu kwa kupenda mno mali na madaraka, mambo ambayo yamekuwa ni chanzo cha
kupotea kwa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya Jamii nyingi Barani
Afrika. Ikiwa kama Jamii itasimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu,
watu wataweza kuishi kwa amani na utulivu.
Askofu Giuseppe Filippi aliwataka
watu waliobahatika kuwa na fedha pamoja na mali, kuonesha upendo na mshikamano na
maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Amewataka pia kupambana
kufa na kupona na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyokwamisha maendeleo ya watu
na hivyo kusababisha kinzani na migogoro ya kijamii. Mashahidi wa Uganda walionesha
moyo wa upendo na ukarimu kwa maskini na wahitaji, wakatoa mali yao kwa ajili ya kuwasaidia
wagonjwa na kueneza Habari Njema ya Wokovu.
Rais Yoweri Kaguta Museven wa Uganda
amewataka viongozi wa kidini nchini Uganda kujifunga kibwebwe kushiriki katika mapambano
dhidi ya umaskini nchini Uganda kwa kuchangia kwa hali na mali sera, mipango na mikakati
ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza kipato cha familia!