Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Pentekoste kwa Mwaka
2014, linawatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, upendo na amani inayobubujika
kutoka kwa Yesu Kristo. Kuna mengi yanayoapswa kuadhimishwa kwa kushikamana kwa pamoja,
ili kuleta mageuzi katika kazi ya uumbaji, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili
aweze kuumba tena sura ya nchi kutokana na wasi wasi na mashaka yanayoendelea kujidhihirisha
katika ulimwengu mamboleo.
Mazingira yanapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa
kwa ajili ya mafao ya wengi, kwani kuna uhusiano wa karibu kati ya uharibifu wa mazingira
na madhara yanayojitokeza katika maisha ya binadamu na jamii inayomzunguka na kwamba,
kwa sasa maisha ya mwanadamu yako hatarini pengine kuliko wakati mwingine wowote katika
historia ya binadamu!
Lengo la Pentekoste kadiri ya mpango wa Mungu ni kuleta
umoja na mshikamano kutokana na mgawanyiko wa watu katika sura ya dunia uliosababishwa
na kuvurgika kwa lugha. Utekelezaji wa ahadi hii ya Mungu inaonesha kana kwamba, inakinzana
na uhai wa binadamu katika nyakati hizi. Lakini ikumbukwe kuwa uwepo wa Mungu katika
maisha ya mwanadamu ni chemchemi ya utakatifu, maendeleo na utambulisho wake, mambo
ambayo kwa sasa yako hatarini.
Kwa njia ya Pentekoste, ukweli kuhusu uumbaji
unajionesha kwa namna ya pekee katika sala ambayo inamwonesha Mungu kuwa kweli ni
Mungu wa Uhai anayependa kuwaelekeza watu katika haki na amani. Baraza la Makanisa
linamwomba Roho Mtakatifu aweze kuwashukia, kujidhihirisha kati yao na kuwawezesha
kuwa wamoja!