2014-06-07 09:47:58

Mna haki na wajibu wa kushiriki utume na maisha ya Kanisa!


Waamini walei wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, wamepewa karama mbali mbali na Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili kusaidia kueneza ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda makini unayoyatakatifuza malimwengu. Waamini walei watambue kwamba katika Kanisa kuna tofauti za huduma, lakini utume ni mmoja. Waamini walei wanashiriki pia ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo, unaowachangamotisha kutoka kifua mbele pasi na woga ili kuwatangazia watu Injili ya Furaha kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Haki na wajibu wa waamini walei inabubujika kutokana na muungano wao na Kristo ambaye ni kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, wanashirikishwa mapendo ya Kristo, kiini cha utume wote wa Kanisa. Utume huu unatekelezwa katika imani, matumaini na mapendo, fadhila ambazo Roho Mtakatifu hueneza mioyoni mwa Wanakanisa wote. Mapaji ya Roho Mtakatifu waliyokirimiwa waamini ni kwa ajili ya mafao ya wanadamu na ujenzi wa Kanisa la Mungu.

Kutokana na wajibu na haki hizi msingi kwa waamini walei, hivi karibuni, Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania amewataka waamini walei nchini Tanzania, kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Askofu mkuu Padilla ameyasema hayo wakati wa hija yake ya kichungaji Jimbo Katoliki la Same aliyoifanya kwa mwaliko wa Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki la Same. Katika ziara hii, Askofu mkuu Padilla alitabaruku Makanisa mawili Jimboni Same, kielelezo cha waamini kujisadaka katika kulitegemeza Jimbo lao.

Askofu mkuu Padilla amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa limebahatika kuwa na watu wenye karama na mapaji mbali mbali yanayopaswa kutumiwa kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Kuna watu ambao wameajiriwa, kuna wakulima wanaojitaabisha kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula na kuna vijana, wazee na watoto; wote hawa wanahitaji kujenga msingi thabiti wa umoja na mshikamano, chachu muhimu sana katika Uinjilishaji Mpya, changamoto inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika nyakati hizi za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Waamini wa Jimbo Katoliki la Same wametakiwa kuwa imara na thabiti katika imani, matumaini na mapendo; huku wakidumu katika: maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa bila kusahau kuwagusa maskini na wanyonge kwa njia ya upendo na mshikamano unaoponya na kufariji! Waamini walei wanatumwa kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili, mayofu na matakatifu; maisha yenye mvuto na mashiko kwa jirani. Wajitahidi kuwatafuta ndugu zao waliopotea katika imani, kwa kuwapenda, kuwalinda na kuwapatia matumaini mapya ya maisha!

Askofu mkuu Francisco Padilla katika ziara yake ya kikazi Jimboni Same, ametoa pia Sakramenti ya Ubatizo na kuwaimarisha Wakristo kwa Sakramenti ya Kipaimara inayowawezesha waamini kumpokea Roho Mtakatifu, tayari kulinda na kueneza imani sehemu mbali mbali za dunia. Askofu mkuu Padilla ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Makleri Jimbo Katoliki la Same pamoja na kubariki Pango la Bikira Maria lililoko kwenye eneo la Kanisa kuu la Kristo Mchungaji mwema, Jimbo la Same, Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.