Kardinali John Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anasema kwamba, vitendo vya
kigaidi vinavyoendeshwa na Kikundi cha Boko Haram bila kudhibitiwa kwa kuhofia kwamba,
kwa kupambana na Boko Haram kuna maanisha kupambana na waamini wa dini ya Kiislam
ni kuwa na tafsiri finyu ya ukweli wa mambo. Hakuna upinzani kati ya Wakristo na Waisla,
vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kukishughulikia Kikundi cha Boko Haram kama
kikundi cha kigaidi na wala si dhehebu la dini ya Kiislam!
Mahakama ya Kijeshi
nchini Nigeria imewatia hatiani baadhi ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama
ambao wamekuwa wanajihusisha na uuzaji wa silaha za moto kwa Boko Haram, ingawa taarifa
hizi zimekanushwa na Kamanda mkuu wa Jeshi la Nigeria anasema Kardinali Onaiyekan.
Lakini ana uhakika kwamba, iko siku wananchi wa Nigeria watafahamu ukweli wa mambo
na wapi Boko Haram wanapata silaha za kufanya mashambulizi kiasi cha kutetekeza kijiji
kizima. Kama habari hizi ni za kweli, basi wanajeshi wenye uchu wa mali na utajiri
wa haraka haraka wanalichafua jeshi na ndiyo maana Serikali inashindwa kuwathibiti
kutokana na vitendo vinavyoendelea kusababisha madhara makubwa kwa usalama wa watu
na mali zao!
Kardinali Onaiyekan anasema, Boko Haram si vita kati ya Wakristo
na Waislam na wale wanaotazama tatizo hili katika mwelekeo kama huu wanakosema. Boko
Haram ni kikundi cha kigaidi, kinachopaswa kushughulikiwa kadiri ya sheria za nchi
ya Nigeria pamoja na sheria za kimataifa. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaundwa na
waamini wa dini mbali mbali, kumbe, ikiwa kama udini unatumika kwa ajili ya kuwakingia
kifua Boko Haram hapa ni hatari kubwa na ukiukwaji wa maadili na kanuni za Kijeshi
na kwamba, wahusika wanapaswa kushughulikiwa kikamilifu!
Boko Haram licha ya
mikakati inayoendeshwa na Nigeria kwa kusaidiana na Jumuiya ya Kimataifa, lakini bado
linafanya mashambulizi kwa watu wasiokuwa na hatia. Wasichana wa shule waliotekwa
nyara hivi karibuni bado hawajaachiliwa huru, hii inaonesha kwamba, Serikali inashindwa
kutawala baadhi ya maeneo ya ardhi yake, jambo ambalo linatia shaka sana.
Kuna
haja kwa Nigeria kufanya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi ili kuamua mustakabali
wa Nigeria kwa sasa na kwa siku za baadaye. Mikakati ya kijeshi peke yake haitoshi,
kumbe kuna haja ya kuwa na sera na mikakati mipana zaidi kwa kushugulikia pia tatizo
la rushwa na ufisadi, mambo ambayo pengine yanagumisha mapambano dhidi ya Kikundi
cha kigaidi cha Boko Haram.