Ni siku nyingine tena tunapokutana katika meza ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha
sherehe ya Pentekoste, sherehe ambayo katika kalenda ya litrujia huja siku hamsini
baada ya pasaka.
Ni sherehe
ambayo wakristu humshangilia Kristu mfufuka katika Roho Mtakatifu na kufurahia ukombozi
ambao umeletwa na Kristo mwenyewe. Katika sherehe ya Pentekoste fumbo la pasaka hukamilika
maana ni katika sikukuu hii Roho Mtakatifu hulishukia Kanisa ili likaendeleze kazi
ya Kristu bila woga, likiwa na nguvu za kimungu. Ni sherehe ambayo kwayo Roho Mtakatifu
huthibitisha muungano wetu na Mungu. Ujumbe wa Neno la Mungu unalala katika Roho Mtakatifu
kuwa sheria mpya na nguvu ya Wakristu, taifa jipya lililoshikamana katika upendo na
Mungu.
Katika somo la kwanza toka kitabu cha Matendo ya Mitume, tunaona Mitume
wakiwa mahali pamoja na ghafla upepo na uvumi, ndimi za moto zinawashukia. Wote wakajazwa
na Roho Mtakatifu na kuanza kunena kwa lugha mbalimbali. Wanapokea nguvu ya Mungu
na hivi wanaweza kutenda matendo ya ajabu kwa mataifa.
Tunasikia pia, watu
waliwashangaa Mitume kwa kuwa watu hawa waliweza kusikia na kuelewa ujumbe uliokuwa
ukihubiriwa na Mitume katika lugha zao. Hii ni ajabu maana baada ya mnara wa Babeli
(Mw.11:1-9) watu hawakuweza kuelewana kiurahisi. Kumbe Roho Mtakatifu ni muunganishi
wa taifa jipya la Mungu ambalo ni tunda la ufufuko.
Ishara mbalimbali tulizozisikia
hapo juu zatupa mwanga ili kuweza kuelewa vema tendo la kushuka kwa Roho Mtakatifu.
Uvumi wa upepo na ndimi za moto zinatupa mazingira ya sheria ya zamani, yaani wakati
sheria ya zamani ilipokuwa ikitangazwa tunaposoma katika kitabu cha Kutoka, kulitokea
alama hizo (Kut.19:16).
Wakati Musa alipokuwa akipokea sheria ya Mungu maneno
ya Mungu yalibadilika na kueleweka katika ndimi sabini za moto (Kut.20:18). Hili lilimaanisha
kuwa sheria hii ni kwa ajili ya watu wote duniani. Luka anapoandika jambo la kushuka
kwa Roho Mtakatifu anatumia alama zilezile ili aweze kueleweka kwa urahisi kwa walengwa
wa Neno la Mungu.
Mwinjili Luka anatumia alama ya lugha nyingi akionesha utamaduni
uliokwishajengeka katika Kanisa la mwanzo, yaani watu walipompokea Roho Mtakatifu
walinena kwa maneno mapya wakimsifu Mungu. Alama hii ni kielelezo cha umoja wa Kanisa,
yaani Kanisa lililo kwa ajili ya wokovu wa wote. Injili ni kwa ajili ya mataifa yote,
inatupilia mbali mipaka ya rangi, kijiografia, lugha na mambo yote yaletayo hatari
na kuvuruga umoja wa taifa la Mungu.
Ni kwa njia ya Pentekoste wale wote waliotawanyika
wanakusanywa tena kwa sheria mpya yaani, sheria ya mapendo inayounda familia mpya
ya Mungu. Sheria hii inaandikwa mioyoni mwa watu.
Mtakatifu Paulo anapowaandikia
Wakorinto anawakumbusha kuwa karama walizopewa si kwa ajili ya ubinafsi bali kwa ajili
ya umoja. Anawaambia kuwa Roho ni mmoja na karama ni mbalimbali kwa ajili ya shughuli
za misioni, kwa ajili ya kupamba upendo uleule. Anawakumbusha hilo akitumia alama
ya mwili mmoja ulio na viungo mbalimbali vyenye shughuli mbalimbali kwa ajili ya mwili
huo mmoja. Mwishoni anataka karama ziwe ni chanzo cha mapendo katika familia yao ndiyo
Kanisa.
Hivi leo katika jamii mbalimbali kuna machafuko kwa sababu ya kila
mmoja kuona karama aliyonayo ni kwa ajili yake mwenyewe na si kwa ajili ya jumuiya
yake. Yafaa kuepuka shida hii mapema ili jumuiya yetu ikae kwa amani.
Katika
injili mwinjili Yohane anatangaza amani ya Kristu ambayo ni zawadi ya ufufuko na ni
msingi wa umisionari. Si tu msingi wa umisionari bali pia ni msingi wa upatanisho
na furaha katika familia ya Mungu maana baada ya kuwapatieni amani atawatuma ulimwenguni
kwa ajili ya kazi ya kitume. Katika utume, Mitume wanaalikwa kuwaondolea watu dhambi
zao.
Hawewezi kuondolea dhambi bila Roho wa Mungu na hivi kabla anawavuvia
Roho huyo. Kumbe mpendwa kushuka kwa Roho Mtakatifu ni nguvu ya ondoleo la dhambi
ni amani na furaha ya taifa la Mungu, ni mkazo wa umisionari kazi ya Kristu.
Roho
Mtakatifu anashuka kwa ajili ya kubadili maisha yetu yawe maisha mapya, yawe ni maisha
kwa ajili ya kuwafariji walio katika taabu mbalimbali. Basi ni wajibu wetu sisi tuliompokea
kwa njia ya sakramenti kuweka maisha yetu kama kielelezo cha maisha mapya, maisha
yampendezayo Mungu na watu. Tukishampokea Roho Mtakatifu hatutaweza tena kuangalia
mambo ya chini bali yaliyo ya juu. Ndiyo kusema Roho wa Bwana akishaujaza ulimwengu
huunganisha viumbe vyote kwa ajili ya umoja kamili na Mungu.
Mpendwa katika
siku ya leo tuliombee Kanisa ili liwe kielelezo cha amani na upendo na mshikamano.
Tuwaombee wote waliojiweka wakfu katika Roho Mtakatifu wakatimize kazi yao ya wakfu
kwa furaha na amani. Ninakutakieni sherehe njema na mwendelezo mzuri wa maisha ya
furaha. Ninakukumbusha kuwa leo Mama Kanisa anahitimisha kipindi cha Pasaka. Tumsifu
Yesu Kristo.
Tafakari imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.