Jumuiya ya Kimataifa inaposherehekea kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kusitishwa kwa
Vita kuu ya Pili ya Dunia, viongozi wa Kanisa nchini Ufaransa wanaadhimisha tukio
hili kwa njia ya sala, kwa kuwakumbuka askari wote waliojisadaka kwa ajili ya kutetea
haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko katika
ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican
kwenda kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa anasema kwamba, anaungana na wote
wanaoendelea kuombea amani bila kuwasahau askari wote waliopoteza maisha kutokana
na Vita kuu ya Pili ya Dunia.
Ni wajibu wa vijana wa kizazi kipya kutambua
na kuheshimu sadaka iliyotolewa na mashujaa waliosimama kidete kupinga utawala wa
kinazi, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakiwa na matumaini ya leo na kesho
iliyo bora zaidi.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele
vya watu, ili kweli Injili ya Kristo iweze kushika mkondo wake ili kukuza na kudumisha
amani, udugu na mshikamano. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia hija njema ya amani
wakiendelea kuombewa na Mtakatifu Bernadetha wa Msalaba, Msimamizi mwenza wa Bara
la Ulaya.