2014-06-06 14:53:16

Askari ni wito wa huduma!


Jubilee ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi Italia, maarufu kama Carabinieri ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya historia ya Jeshi la Nchi ya Italia, inayojikita katika mshikamano, imani, majitoleo kwa ajili ya mafao ya wengi. Jeshi hili limeenea sehemu mbali mbali za Italia na ni sehemu muhimu sana katika ujenzi wa amani na utulivu kati ya watu. Ni Jeshi ambalo liko karibu na raia na hasa zaidi maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ni wito wa huduma!

Ni hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Jeshi la Carabinieri waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican siku ya Ijumaa tarehe 6 Juni 2014, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, huduma yao inajikita katika ulinzi wa watu na mazingira; utekelezaji wa sheria; amani na utulivu pamoja na kuzingatia mafao ya wengi. Ni kazi inayowawajibisha kulinda na kutetea haki na dhamana ya mtu binafsi na jamii husika, ili kila mtu na jamii iweze kujieleza na kujibu wito wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ni utume unajioelekeza katika huduma ya kila siku inayohitaji imani na heshima inayotolewa na wananchi katika ujumla wao! Utume huu unahitaji kwa namna ya pekee uwepo, uvumilivu, sadaka na dhamana. Ni mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu kama walivyofanya watangulizi wao, kiasi kwamba, leo hii wanaheshimiwa na Kanisa kama Watumishi wa Mungu. Hawa ni kama vile Salvo D'Acquisto akiwa na umri wa miaka 23 alijisadaka kwa ajili ya watu waliokuwa wanadhulumiwa na kuteswa na utawala wa Kinazi.

Baba Mtakatifu anawaomba Carabinieri kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao katika utulivu, ukarimu na ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya kifamilia. Anawapongeza kwa kujitosa katika kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani ndani na nje ya Italia, hasa katika nchi zile ambazo bado vita na mtutu wa bunduki unatawala. Huu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika ubinadamu kwa kujitoa zaidi kwa maskini na watu wenye shida.

Baba Mtakatifu amewaweka Carabinieri chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria mwaminifu, wamkimbilie wakati wa kuchoka na magumu; wanapokosa amani na usalama, kwani Bikira Maria atawasaidia kwa kuwaombea kwa Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo. Baba Mtakatifu anasema kwamba, tarehe 13 Septemba 2014 atafanya hija ya kiroho kwa kutembelea makaburi ya Askari huko Redipuglia, Gorizia, ili kuwaombea Askari wote waliopoteza maisha yao wakati wa vita mbali mbali. Ni kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu Vita kuu ya Pili ya Dunia ilipoanza kutimua vumbi!







All the contents on this site are copyrighted ©.