2014-06-05 07:46:56

Upendo kwa Mungu na jirani!


Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amegusia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukazia zaidi na zaidi kanuni maadili na utu wema; utu na heshima ya binadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia: Yote haya ni kadiri ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki na Kweli za Kiinjili na wala hakuna mabadiliko! RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Francisko anapozungumzia masuala haya kwa unyenyekevu mkubwa kutokana na uzoefu wake katika shughuli za kichungaji kuna baadhi ya watu wanapata hisia kwamba, pengine anataka kubadilisha mafundisho na msimamo wa Kanisa Katoliki katika masuala haya, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, anachofanya ni kuendelea kukazia masuala haya kwa mwelekeo mpya zaidi!

Hivi ndivyo anavyofafanua Kardinali Leo Burke, Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Vatican. Anasema, Baba Mtakatifu si mtu anayetaka kurudia rudia mambo kuhusu utoaji na vizuia mimba, ndoa za watu wa jinsia moja, jambo analolipatia kipaumbele cha pekee ni upendo kwa watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bila ubaguzi na kwa njia hii, mafundisho ya Kanisa yanaweza kupokelewa vyema zaidi na kwamba, ameendelea kuzungumzia masuala haya katika nyanja mbali mbali, jambo la msingi ni kufungua macho, masikio na mioyo ili kuupokea ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko.

Ni kiongozi anayejielekeza zaidi katika mikakati ya upendo wa kichungaji, hivi ndivyo anavyopaswa kueleweka, kwani anataka kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu; anapenda kuwaona watu wanaguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao, ili kudumisha mshikamano wa upendo kati ya watu pamoja na kukoleza misingi ya haki, amani na utulivu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wajitahidi kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kwa njia huruma, upendo na mshikamano, watu wanaweza kumwona Kristo na Kanisa lake na hatimaye, kukubali kupokea mwaliko wa kumfuasa. Changamoto kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya ni ushuhuda wa utakatifu wa maisha, mwaliko kwa kila mwamini.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuondoa vikwazo vinavyowanyima fursa ya kukutana na Yesu, ili waweze kuonja, upendo na huruma yake na hivyo kuwa tayari kuanza hija ya toba na wongofu wa ndani kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na Kanisa lake. Waamini wajitahidi kusimika maisha yao katika “Heri za Mlimani” ambazo ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wanafunzi wake. Wajenge utamaduni wa kukutana na kuzungumza na Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti; mambo yanayomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji!

Huu ndio mwaliko wa Uinjilishaji Mpya, yaani changamoto ya kumtangaza Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu si tu kwa maneno bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu! Uinjilishaji Mpya unajikita katika Injili na Mapokeo ya Kanisa. Watu waoneshe ujasiri wa kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani!

Watu watubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuanza mchakato wa utakatifu wa maisha. Waamini wasilegeze kamba katika maadili hasa kwa mambo ambayo leo hii yanayonekana kuwa ni ya kawaida katika maisha ya watu wengi. Amri za Mungu ni mambo ya kuzingatiwa.

Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko anatoa mwaliko kwa waamini kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaojielekeza katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upendo, tayari kukumbatia kwa imani na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, ili kulijenga Kanisa la Kristo na kuendelea kumshuhudia Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Yesu awe ni nguzo thabiti katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!

Hivi ndivyo Kardinali Raymond Leo Burke anayofafanua kuhusu uelewa Papa Francisko katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.