2014-06-05 16:01:07

Kanisa liwe ni sura ya furaha na ukarimu kwa Zingari


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Juni 2014 amekutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa linalojadili kuhusu mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Zingari, kongamano linaloongozwa na kauli mbiu "Kanisa na Zingari: Kutangaza Injili pembezoni mwa jamii. Hii ni kumbu kumbu kati ya Jumuiya ya Waamini na Zingari na historia inayolenga watu kukutana na kufahamiana ili kwa pamoja waweze kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya changamoto zinazojitokeza kati shughuli za kichungaji lakini zaidi katika Uinjilishaji Mpya.

Zingari ni watu ambao wanaishi pembezoni mwa Jamii na mara nyingi ni kundi ambalo halipendwi na wengi na wanawaangalia kwa mashaka makubwa. Kimsingi hakuna sera makini za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazojielekeza kwa ajili ya kuasaidia watu hawa. Zingari nao wanahamasishwa kushiriki katika kuchangia katika mafao ya wengi, kwa kuwajibika, kutekeleza nyajibu zao na kuendeleza haki msingi za wote.

Ukosefu wa miundo mbinu makini ya elimu na majiundo ya kitamaduni ni kati ya mambo ambayo yanaweza kuwatumbukiza baadhi ya watu ndani ya jamii katika lindi kubwa la umaskini, magonjwa, ubaguzi katika soko la ajira pamoja na kutothaminiwa. Ikiwa kama mambo haya ni kati ya madonda makubwa ya kijamii, basi wanyonge watajikuta wakitumbukizwa kwa urahisi katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, kwani hawa ni watu ambao hawana ulinzi na usalama wa kutosha.

Zingari ni kati ya makundi ya watu wanaoendelea kutumbukizwa katika utumwa mamboleo, kwani hawashirikishwi na wala utu wao hauheshimiwa kiasi kwamba, wanashindwa kuishi kama raia wengine.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linatumwa kuwatangazia watu Injili ya Furaha na hii ndiyo changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa ajili ya maskini na wote wanaosukimzwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa lioneshe mshikamano wa upendo kwa kufuata ushuhuda ulioneshwa na Yesu Kristo, Mwana mpendwa wa Baba.

Mshikamano huu uungwe mkono na taasisi za kitaifa na kimataifa, kwa kubainisha miradi na mbinu za kuboresha maisha. Utu na heshima yao vipewe msukumo wa pekee pamoja na kuibua mbinu na mikakati mipya kutoka katika medani mbali mbali za maisha sanjari na kuweka mipango ya kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa kutokana na changamoto zinazojitokeza katika mtindo wa madhulumu, ukandamizaji na hata wakati mwingine utumwa!

Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe na wadau mbali mbali kujielekeza zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ya mwanadamu. Zingari wapate ndugu wanaowapenda kama Kristo alivyowapenda wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa liwe kweli ni sura ya furaha na ukarimu kwa Zingari.







All the contents on this site are copyrighted ©.