2014-06-05 11:11:27

Jengeni umoja wa kitaifa na pambaneni na rushwa na ufisadi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wanasiasa kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kupambana kufa na kupona na rushwa pamoja na ufisadi unaovuruga misingi ya haki na amani nchini Kenya. Ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu Martin Kivuva, Mwenyekiti wa Idara ya Upashanaji Habari, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, iliyofanyika hivi karibuni.

Chuki na uhasama ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuwajengea hofu kubwa wananchi wa Kenya. Kumbe, kuna haja kwa viongozi mbali mbali nchini Kenya kujitahidi kujenga misingi ya haki, amani na utulivu. Serikali, wanasiasa na watunga sera wabainishe mikakati itakayowawezesha wananchi wa Kenya kupambana na umaskini wa hali na kipato pamoja na kuwa na matumizi bora ya rasilimali iliyopo, ili iweze kutumika kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya.

Kenya ina idadi kubwa ya Wakristo wanaohamasishwa kujenga utamaduni wa kuwa waaminifu na wa kweli na kamwe wasipokee wala kutoa rushwa kwani rushwa ni adui mkubwa wa haki.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawapongeza wadau mbali mbali wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika vyombo vya upashanaji habari nchini Kenya katika mchakato wa ujenzi wa amani na mshikamano wa kitaifa hasa mara tu baada ya Kenya kujipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Ni vyema ikiwa kama maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yatatumika pia kuendeleza tunu msingi za maisha ya wananchi wa Kenya!







All the contents on this site are copyrighted ©.