Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Alhamisi ameongoza Ibada ya Misa Takatifu
kwa ajili ya kumsindikiza Kardinali Simon Lourdusamy katika makazI ya uzima wa milele,
akiwa na umri wa miaka 90 ya kuzaliwa, kiongozi aliyejisadaka tangu akiwa kijana kwa
ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Aliwaongoza, aliwafundisha na kuwatakatifuza
watu wa Mungu Jimbo kuu la Pondicherry na Bangalore; akaitwa na Mtumishi wa Mungu
Papa Paulo VI kwa ajili ya kusaidia utume katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
wa Watu. Kwa miaka kadhaa alijisadaka kwa ajili ya Kanisa hadi pale alipokumbwa na
ugonjwa, akaendelea kulitumikia Kanisa kwa njia ya sala na mateso, huku akionesha
uvumilivu mkubwa!
Kardinali Sodano anasema, kila wakati Kanisa linapoadhimisha
Ibada ya Mazishi linapenda kuwaimarisha watoto wake katika imani kuhusu maisha ya
uzima wa milele ambako hakutakuwa na misiba wala majonzi tena na kwamba, binadamu
hapa duniani ni msafiri wala hana makazi ya kudumu, makazi yake yameandaliwa mbinguni,
jambo la msingi ni kwa waamini kuendelea kumwamini Yesu Kristo.
Mwishoni mwa
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Simon Lourdusamy,
Baba Mtakatifu Francisko aliungana na Familia ya Mungu iliyokuwa imekusanyika kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya Ibada ya maziko, ili Marehemu
Kardinali Lourdusamy aweze kusindikizwa na hatimaye kupokelewa na Malaika mbinguni
ili aweze kupumzika kwa amani. Amina.