Umuhimu wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa
Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano maalum
na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea
kutoa kipaumbele cha pekee katika kudumisha umoja na mshikamano ndani ya Kanisa kwa
kukazia umuhimu wa Sinodi za Maaskofu katika maisha na utume wa Kanisa.
Kutokana na
dhamana hii nyeti ndani ya Kanisa ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 30
Mei 2014 amemweka wakfu Askofu Fabio Fabene katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Askofu Fabene alianza utume
wake mjini Vatican kunako mwaka 1997 na tarehe 8 Februari 2014 akateuliwa na Baba
Mtakatifu Francisko kuwa katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. Anakumbuka mchango
mkubwa uliofanywa na Marehemu Kardinali Bernardin Gantin katika Baraza la Kipapa la
Maaskofu kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kifamilia na ushirikiano katika kutekeleza
majukumu mbali mbali ndani ya Baraza.
Hii ndiyo changamoto anayotaka kuifanyia
kazi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuhakikisha kuwa, Sinodi za Maaskofu
zinakuwa ni kama Familia. Baraza la Maaskofu limejitahidi kuangalia na hatimaye kupitisha
Katiba za Mabaraza ya Maaskofu kadiri ya miongozo iliyotolewa na Mama Kanisa na kwamba,
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha, “Evangelii
gaudium” anakazia kwa namna ya pekee umoja na mshikamano katika maisha na utume wa
Kanisa.
Askofu Fabio Fabene si mgeni sana katika kuta za Vatican, kwani wakati
wa mchakato wa kumtafuta kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki baada ya Baba Mtakatifu
Benedikto XVI kung’atuka kutoka madarakani alishirikiana kwa karibu zaidi na Kardinali
Lorenzo Baldiselli, kumbe, kama Katibu wa Sinodi za Maaskofu anapenda kushirikisha
mang’amuzi na uzoefu wake kutoka katika Baraza la Kipapa la Maaskofu.
Mtumishi
wa Mungu Papa Paulo VI kunako tarehe 15 Septemba 1965 alianzisha maadhimisho ya Sinodi
za Maaskofu kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu katika
utekelezaji wa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Haya
ndiyo mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuyaona yakitendeka ndani
ya Kanisa wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu Katoliki.
Sinodi maalum
ya Maaskofu kuhusu Familia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2014 mjini Vatican itaangalia
fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kuikabilia familia ya mwanadamu. Wanafamilia
watapewa nafasi ya kujadili kuhusu mustakabali wa maisha na utume wao ndani ya Kanisa,
ili hatimaye, kuwasaidia Maaskofu kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu,
ili kweli Kanisa liweze kuendelea kutangaza Injili ya Familia katika ulimwengu mamboleo.
Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia unaendelea
vyema. Baba Mtakatifu anaitaka Familia ya Mungu kuwajibika barabara katika kutangaza
Injili ya Familia. Kila Askofu mahalia anatambua dhamana na utume wake kwa Kanisa
mahalia lakini pia anaungana na Kanisa zima kwa ajili ya ustawi na mafao ya Familia
ya Mungu. Hii ni changamoto kubwa kutoka katika Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Maaskofu
kama wachungaji wakuu wa Makanisa mahalia wanapaswa kuwa watu na wajenzi wa umoja
na mshikamano, ili kuchangia ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Sinodi za Maaskofu
zinalenga kuimarisha na kukuza umoja na mshikamano kati ya Maaskofu!