Shirika la kuhudumia la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto wadogo UNICEF kwa kuungana
na UNFPA yana unga mkono kampeni iliyozinduliwa hivi karibuni ya Umoja wa Nchi za
Kiafrika ya kupambana na ndoa za utotoni ambazo zinazidi kuongezeka kwa wingi Barani
Afrika na hivyo kusabababisha majanga makubwa kwa watoto zaidi ya millioni 17 wanaotoka
Barani Afrika.
Takwimu zinaonesha kwamba, Niger, Chad, Jamhuri ya watu wa
Afrika ya Kati, Guinea, Msumbiji, Mali, Burkina Faso, Sudan ya Kusini na Malawi zinaongoza
kwa ndoa za utotoni Barani Afrika. Changamoto hii iliyotolewa na Umoja wa Afrika inapaswa
kuungwa mkono na wapenda amani duniani anasema Bwana Martin Mogwanja, Mkurugenzi msaidizi
wa UNICEF wakati akichangia mada kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni mjini Addis
Ababa.
Kampeni hii iwasaidie watoto kukua na kukomaa hadi watakapofikia umri
wa miaka kumi na minane inayoruhusiwa kisheria kuweza kufanya maamuzi kuhusu maisha
yao badala ya kudumazwa katika ndoa za utotoni ambazo zimeendelea kuwa na madhara
makubwa kwa watoto hawa na familia wanazounda! Kwa mara ya kwanza katika historia,
Jumuiya ya Kimataifa inaonesha utashi wa kutaka kupambana na ndoa za utotoni ili kuimarisha
afya, matumaini na haki msingi za watoto Barani Afrika.
Kampeni hii iliyozinduliwa
hivi karibuni itadumu kwa kipindi cha miaka miwili katika ngazi ya kitaifa kwa mataifa
kumi. Lengo ni kuwawezesha wananchi kufahamu madhara ya ndoa za utotoni na hivyo wanasiasa
na vyombo vya sheria kuwajibika ili kukomesha vitendo hivi.