Mkutano wa viongozi wa kidini kuhusu mikakati ya maendeleo endelevu!
Kamati ya ufundi kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madgascar,
SECAM, hivi karibuni imemaliza kikao chake cha siku tatu kilichokuwa kinafanyika Jijini
Kampala, Uganda kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa viongozi wa dini kuhusu maendeleo
endelevu baada ya mwaka 2015 unaotarajiwa kufanyika mjini Entebbe, Uganda, kati ya
tarehe 1- 2 Julai 2014.
Mkutano wa
maendeleo endelevu huko Entebbe unapania pamoja na mambo mengine kuendeleza mchakato
wa mikakati ya Maendeleo ya Millenia baada ya Mwaka 2015, iliyokuwa imebuniwa na Umoja
wa Mataifa. Huu utakuwa ni mkutano wa kujadili mikakati ya maendeleo na matokeo yake
na kwa namna ya pekee, itakuwa ni fursa ya kuweza kuwashirikisha viongozi wa kidini
kutoka Barani Afrika.
Lengo ni kusaidia kuwahamasisha viongozi wa Serikali
na taasisi katika nchi zao kuhusu sera na mikakati inayopania kuendeleza uchumi unaozingatia
masuala msingi katika maisha ya kijamii; ushirikishwaji wa jamii na upatanisho. Mambo
mengine ni kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja
na kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi.
Mkutano wa viongozi wa
kidini Barani Afrika utawahusisha viongozi wa dini ya Kiislam, Kikristo pamoja na
dini mbali mbali zinazopatikana Barani Afrika. Kamati ya ufundi kutoka SECAM imekutana
na kuzungumza na Baraza la majadiliano ya kidini nchini Uganda pamoja na viongozi
wa Serikali ya Uganda ili kujadili kuhusu ushiriki wao pamoja na msaada wa kufanikisha
mkutano wa viongozi wa kidini kutoka Barani Afrika.