2014-06-03 08:34:02

Mapambano ya baa la njaa Barani Afrika!


Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 29 Novemba 2014, litakuwa ni Mwenyeji wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi katika mkutano unaolenga kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mapambano dhidi ya baa la njaa duniani. RealAudioMP3

Huu ni mkutano wa kimataifa unaolijumuisha Shirika la la Misaada la Kanisa Katoliki (OCADES) ambalo ni tawi tanzu la Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Mkutano huu utaongozwa na kauli mbiu “Mkakati wa kuondokana na baa la njaa Ukanda wa Sahel”.

Mkutano huu utawashirikisha wajumbe kutoka nchi za Afrika Magharibi na nje ya eneo hili kwa mwaliko maalum. Wadau mbali mbali wanaojihusisha na haki msingi ya chakula katika ngazi ya kimataifa wamealikwa pia. Hii itakuwa ni nafasi nzuri kwa Kanisa Afrika Magharibi kufanya upembuzi yakinifu kuhusu baa la njaa na mikakati ya Kanisa katika mapambano haya sanjari na kufanya mabadiliko msingi katika maisha ya jamii, ili baa la njaa usiwe tena ni wimbo usiokuwa na kiitikio! Watu wawajibike katika kujihakikishia usalama wa chakula.

Itakumbukwa kwamba, tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kimataifa inayotaka kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na uhakika wa usalama wa chakula, iliyozinduliwa na Caritas Internationalis kunako Desemba 2013 na Baba Mtakatifu Francisko akatoa ujumbe kwa njia ya video, akiwahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika kampeni hii kwani, baa la njaa bado ni kashfa kubwa duniani.

Inakadiriwa kwamba, kuna watu billioni moja wanaokabiliwa na baa la njaa sehemu mbali mbali za dunia, ingawa kuna uzalishaji mkubwa wa chakula! Ubinafsi, uchoyo na utandawazi wa watu kutoguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao ni chanzo kikubwa cha kuenea kwa baa la njaa duniani!








All the contents on this site are copyrighted ©.