Kimbilieni huruma na upendo wa Mungu kwani mnaye Mwombezi!
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukimbilia kwenye kiti cha huruma na upendo
wa Mungu usiokuwa na kifani mara tu wanapoanguka dhambini kwani kuna Mwombezi ambaye
daima yuko mbele ya Mwenyezi Mungu kuwaombea na kuwatetea, huyu si mwingine bali ni
Yesu Kristo Mkombozi wa dunia! Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati wa mahubiri yake
kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 3 Juni
2014, Kanisa linapoadhimisha Kumbu kumbu ya Mashahidi wa Uganda.
Baba Mtakatifu
anasema, Yesu si tu kwamba, anazungumza na kuwatetea mbele ya Baba yake wa mbinguni,
lakini zaidi anawapenda na amegharimia ukombozi wa binadamu kwa njia ya mateso, kifo
na ufufuko wake. Madonda matakatifu ya Yesu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu
kwa wakosefu. Yesu baada ya ufufuko wake na kupaa kwenda mbinguni kwa Baba yake ameendelea
kuyatunza mwilini mwake Madonda Matakatifu, ili yaweze kuwa ni alama ya kuwaombea
huruma na msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu.
Madonda Matakatifu ya Yesu ni matokeo
ya dhambi za binadamu, chachu ya huruma na upendo wa Mungu ili kuweza kuwaimarisha
wafuasi wake katika imani na matumaini kama ambavyo Yesu mwenyewe alimwombea Mtakatifu
Petro ili akiishakuimarika katika imani aweze pia kuwaimarisha ndugu zake katika imani
kwa Kristo na Kanisa lake!